Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, amewataka watumishi wa Halmashauri kushiriki mafunzo ya bajeti kwa umakini mkubwa huku akisisitiza kuwekwa kwa vipaumbele vinavyoendana na mahitaji halisi ya idara mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika kikao cha mafunzo ya bajeti kilichofanyika September 30 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Wakil Muhoja aliwataka watumishi hao wa Halmashauri kushiriki kikamilifu kwa lengo la kuhakikisha mpango wa bajeti wa mwaka 2026/2027 unaakisi mahitaji halisi ya idara zote na kuondoa changamoto zilizojitokeza kwenye bajeti iliyopita.

Akizungumza katika kikao hicho Muhoja alieleza kuwa bajeti ijayo inapaswa kuzingatia kukamilisha miradi ya maendeleo, kulipa stahiki za watumishi mbalimbali, pamoja na shughuli mbalimbali za kitaifa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa maafisa watendaji wa kata kuwajibika kikamilifu katika ukusanyaji wa mapato na kuweka nidhamu ya kazi, huku akiwataka kuweka makadirio halisi ya mapato kulingana na mazingira ya maeneo yao.

Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Manispaa ya Songea imetenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Idara ya Mipango Miji pamoja na jengo la Maendeleo ya Jamii. Pia, maboresho ya ukarabati wa ofisi ya Uhasibu unaoendelea, huku bajeti ya mwaka 2026/2027 ikilenga kulipa fidia mbalimbali za ardhi.
Wakili Mhoja alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ni muhimu bajeti zisiwe na mzigo mkubwa wa posho pekee, bali zizingatie pia ununuzi wa vitendea kazi na vifaa vingine muhimu kwa utendaji bora wa idara.
MWISHO.
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Maniispaa ya Songea.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa