Na,
AMINA PILLY,
MWANDISHI ALAT RUVUMA.
13 JULAI 2022.
Wajumbe wa Jumuiya ya tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Ruvuma wamefanya ziara ya mafunzo Mkoani Tanga kwa lengo la kujifunza namna ambavyo Jiji la Tanga linatekeleza shughuli zake za maendeleo.
Ziara hiyo ilifanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 Julai 2022 na kuongozwa na Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Ruvuma Kelvin Mapunda pamoja na wajumbe mbalimbali kutoka Mkoani Ruvuma.
Akizungumza katika ziara hiyo Katibu wa ALAT Mkoa wa Ruvuma Grace Quintine alibainisha kuwa lengo la kufanya ziara hiyo ni kujifunza namna ya uendeshaji wa mradi wa dampo, upangaji wa miji, ukusanyaji wa mapato na agenda za lishe, kutembelea fursa za bomba la mafiuta pamoja na kutembelea mapango ya Amboni.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Sipora Liana alisema ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri yake unategemea vyanzo vya mapato mbalimbali ikiwemo na viwanda, leseni za biashara pamoja na service levy.
Aliongeza kuwa kila mkuu wa Idara katika Halmashauri hiyo ana wajibu wa kusimamia vyanzo vyake vya mapato pamoja na kupanga mikakati ya namna ya ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ambayo yanasaidia katika kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wa usafi wa mazingira Sipora alibainisha kuwa ni wajibu wa kila mtendaji wa kata na mtaa kuhakikisha anasimamia usafi katika eneo lake ambapo kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga wamefanikiwa kuweka mazingira ya Jiji hilo katika hali ya usafi unaoridhisha.
Aliongeza miongoni mwa mikakati waliyojiwekea katika kutekeleza suala la upangaji wa miji ni pamoja na kuhakikisha mji unakuwa safi muda wote, kupaka rangi nyumba za mjini kila baada zinapokuwa zimechakaa.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga Abdulrahman Shiloow alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia mapato ya ndani Halmashauri ya Jiji la Tanga imejenga madarasa 100 kwa shule za msingi na sekondari, vituo vya afya 6 pamoja na ofisi za kata 5 ambapo gharama za kila ujenzi wa miradi hiyo ilitokana na fedha za mapato ya ndani.
Shiloow alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya jiji la Tanga imejipanga kukusanya fedha za mapato ya ndani shilingi Billion 18 ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa Jiji waliojiwekea.
Akitoa tathimini ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, kaimu Mweka hazina Richard Mtelewa alieleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 bajeti ya makusanyo ya fedha ilikuwa ni shilingi Billion 15.3 ambapo Halmashauri ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Billion 15.6 sawa na asilimia 102%.
Mussa Alibainisha kuwa hadi sasa Halmashauri hiyo imejikita katika ukusanyaji wa mapato kwa wafanyabiashara wakubwa pamoja na kiwanda cha tofali ambacho kinamilikiwa na Halmashauri hiyo.
Kwa upande wao wajumbe wa ALAT Mkoani Ruvuma wametoa shukrani kwa uongozi wa Halamshauri ya Jiji la Tanga kwa mapokezi pamoja na elimu waliyoitoa ambapo wameahidi kuyafanyia kazi ili kusaidia uongezaji wa mapato katika Halmashauri zao.
Ziara hiyo ilihitimishwa na wajumbe kutembelea katika eneo la mradi wa dampo pamoja na mapango ya Amboni.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa