Iringa, Tanzania – Ugeni kutoka Chama cha Mamlaka za Serikali za Mitaa (ALAT) Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze umetembelea Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa lengo la kujifunza mbinu bora za ukusanyaji wa mapato kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa mapokezi, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Mhe. Ibrahim Ngwada, alisema ujio wa wageni hao ni ishara ya kuthamini mchango na mafanikio ya Halmashauri hiyo katika nyanja mbalimbali.
"Tunashukuru kwa ujio wenu. Tunaamini mtajifunza mengi kupitia Halmashauri yetu ikiwemo usafi wa mazingira, elimu bora, ufugaji wa kisasa, pamoja na utalii – sekta ambazo Iringa imeendelea kuwa mfano wa kuigwa," alisema Mhe. Ngwada.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, CPA Mwajuma Mohamed, alisema Chalinze ina mapato yanayofikia bilioni 18 kwa mwaka, lakini bado wanaendelea kuboresha mifumo yao ya ukusanyaji mapato ambapo alibainisha kuwa ziara hiyo imelenga kupata maarifa kutoka Iringa ambayo imefanikiwa kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato na miradi endelevu.
Naye Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kelvin Mapunda, alieleza kuwa ziara hiyo inalenga kujifunza jinsi Iringa imeweza kuongeza mapato kupitia miradi ya maendeleo, usafi wa mazingira, pamoja na ujenzi bora wa miundombinu ya ofisi za chama na halmashauri.
Wakati wa ziara yao, wajumbe hao walitembelea kiwanda cha maziwa cha ASAS, mashamba ya mifugo ya ASAS yaliyopo Matembo na Igingilanyi, pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii na uwekezaji ndani ya Manispaa ya Iringa, ambavyo vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza mapato na uchumi wa ndani ya mkoa huo.
Ziara hiyo imeanza kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 30 Mei 2025.
NA;
AMINA PILLY
ALAT RUVUMA.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa