Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) ni taasisi iliyoundwa kikatiba mwaka 1984 na kuanza rasmi kutumika mwaka 1985.
Lengo kuu la ALAT ni kupigania haki za Halmashauri na kuwa sauti moja katika kuleta maendeleo katika maeneo husika.
Katika utekelezaji wa lengo hili, wajumbe wa ALAT Mkoa wa Ruvuma, wakiongozwa na Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Kelvin Mapunda, walifanikiwa kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Nyasa tarehe 28 Februari 2025. Ziara hii ilikuwa na lengo la kuimarisha ufanisi wa miradi na kubadilishana uzoefu wa maendeleo kati ya Halmashauri mbalimbali mkoani Ruvuma.
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Kelvin Mapunda, aliwapongeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Ruvuma kwa kusimamia na kuratibu vyema miradi ya maendeleo. Aliendelea kusema kuwa miradi ya maendeleo inaendelea vyema katika mkoa huo na kwamba juhudi hizo zinaendelea kuongeza maendeleo na ustawi wa jamii.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu katika Shule ya Sekondari, ujenzi wa Bwalo la chakula, pamoja na mradi wa Mfumo wa GOTHOMIS uliofungwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyasa. Miradi hii inatajwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 158.
Katibu wa ALAT Mkoa wa Ruvuma na pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Kharid Khalifa, alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imepokea heshima kubwa kwa kuwa mwenyeji wa wageni kutoka ALAT Mkoa wa Ruvuma, na alisisitiza kuwa ziara hii ni muhimu katika kubadilishana uzoefu na kujifunza miradi ya maendeleo kutoka Halmashauri nyingine.
Miradi iliyoangaliwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa vyenye thamani ya shilingi milioni 72, ujenzi wa Bwalo la chakula, na pia mradi wa Mfumo wa GOTHOMIS katika Hospitali ya Wilaya ya Nyasa. Mfumo huu umekuwa na mabadiliko chanya katika ufanisi wa huduma za afya kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Stewart Nombo, alisisitiza kuwa ziara hii ya ALAT ni muhimu sana kwa sababu inawawezesha kujifunza shughuli mbalimbali za maendeleo. Alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyasa kwa juhudi zake za kuleta maendeleo na kuongeza mapato ya Halmashauri kutoka shilingi bilioni 1.7 hadi bilioni 2.9 ikiwa watafanikiwa kukusanya mapato kikamilifu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Khairu Mussa, alielezea kufurahishwa kwake na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Nyasa. Alisema kuwa ziara hii imewapa nafasi ya kujifunza na ameahidi kutekeleza yale waliyojifunza katika Halmashauri aliyotoka.
Ziara hii ilikamilika kwa mafanikio, ikilenga kuboresha ufanisi wa miradi ya maendeleo na kuongeza ushirikiano kati ya Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma.
IMEANDALIWA NA:
Amina Pilly
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa