ASILIMIA 11 ya watanzania watakuwa ni wazee ifikapo mwaka 2050
Tarehe ya kuwekwa: October 1st, 2018
Tanzania inakadiliwa itakuwa na wazee asilimia 11 ya watu wote nchini ifikapo mwaka 2050, kwa kuwa idadi ya watu inaongezeka kwa kasi kutokana na kuendelea kuboreka kwa huduma za Afya hapa nchini. Hayo yamesemwa na Mratibu wa Huduma za Afya kwa Wazee kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Edward Mung’ong’o wakati akiwasilisha mada kwenye kongomano lililofanyika leo Jijini Arusha kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee, amesema kuwa Mwaka 2002 idadi ya Wazee ilikuwa milioni 1.4, ikiwa ni sawa na 4% ya watu wote yaani Milioni 33.5. Aidha Dkt. Mung’ong’o amesema kuwa kwa sasa idadi ya Wazee hapa nchini inakisiwa kuwa milioni 3 sawa na 5.6% ya watu wote ambao kwa takwimu za sasa Tanzania ina Watu milioni 55. Akizungumzia mafanikio ya serikali katika kuboresha huduma za Afya kwa Wazee Dkt. Mung’ong’o amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Shirika la HelpAge International imepitia na kuboresha Mtaala wa kufundishia.