HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imeanza kutoa malipo kwa njia ya mtandao kwa kaya masikini zipatao 4880 ziliopo katika mpango wa kunusuru kaya masikini(TASAF).
Mratibu wa TASAF katika Manispaa ya Songea, Christopher Ngonyani amesema kati ya kaya hizo kaya 2638 sawa na asilimia 54 zinapokea fedha kwa njia ya mitandao ya simu ambapo 2242 sawa na asilimia 46 bado zinapokea kwa njia ya fedha taslimu.
Amesema katika kipindi cha Januari-Februari 2018 kaya 2242 zimelipwa fedha tasilimu zaidi ya shilingi milioni 88 na kaya 2638 zimelipwa kwa njia ya mtandao zaidi ya shilingi milioni 88 na kufanya jumla ya ziadi ya milioni 176 zimetolewa kwa wanufaika wote katika kipindi hicho.
“Lengo ni kwamba ifikapo Juni 2018 tunarajia kufikia asilimia 90 ya wanufaika wote wa TASAF kulipwa fedha kwa njia ya mtandao wa simu’’,anasisitiza Ngonyani.
Hata hivyo amesema lengo la serikali kuanzisha malipo kwa njia ya mtandao ni,kurahisisha usafirishaji wa fedha kwa usalama wa hali ya juu,kufikisha fedha kwa wakati kwa walengwa na kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi.
Ngonyani anasisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wanufaika wote wa TASAF wanajisajiri kulipwa kwa njia ya mitandao ya simu ili kuepukana na changamoto nyingi ambazo zimejitokeza katika malipo ya fedha taslimu ikiwemo kutolewa malipo hewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akizungumza na wanufaika wa TASAF katika Mtaa wa Mitendewawa Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea amesema serikali iliamua kuanzisha ruzuku ya TASAF ili kumkomboa mwananchi masikini.
Amesema asilimia kubwa ya wanufaika wamejiingiza katika shughuli za uzalishaji mali ikiwemo ufugaji na biashara ndogo ndogo ambapo ametolea mfano kwa wanufaika wa TASAF ambao asilimia 90 wanafuga mifugo mbalimbali.
Mgema anaitaja changamoto ambayo imejitokeza kwa baadhi ya wanufaika wachache wa TASAF wilayani Songea kuwa ni kutumia fedha wanazozipata kwa anasa ikiwemo kunywa pombe hali ambayo inarudisha nyuma azma ya serikali ya kuzikomboa kaya masikini.
Utafiti uliofanywa katika mitaa mbalimbali ambayo wanufaika wamelipwa kwa njia ya mtandao,umebaini kuwa mfumo huo umepata mafanikio makubwa baada ya wanufaika wengi kupata fedha zao,hali ambayo imesababisha wanufaika ambao hawajajisajiri kwenye mfumo huo kuhamasika kujisajiri.
Manispaa ya Songea ni moja kati ya Halmashauri 16 nchini zilizochaguliwa kufanya majaribio ya malipo kwa mtandao wa simu kwa wanufaika wa TASAF ili kuepukana na changamoto zilizokuwa zimejitokeza wa kutumia mfumo wa kulipwa fedha za tasilimu.
Mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF unaendeshwa katika Halmashauri 163 katika nchi nzima.Mpango huu umezinufaisha kaya masikini zikiwemo zile ambazo awali zilikuwa zinapata mlo mmoja kwa siku ambapo hivi sasa zinapata milo mitatu kwa siku.
Taarifa imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Februari 7,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa