Mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kutoa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 kwa asilimia 71 ya lengo kwa mwaka 2018
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma alisema chanjo hiyo ilianza kutolewa mwezi Aprili mwaka 2018 katika Halmashauri nane za Ruvuma.
Alitoa taarifa hiyo jana mjini Songea wakati wa kikao cha kamati ya Afya ya Msingi mkoa kutathamini zoezi la utoaji chanjo hii kwa viongozi wa Mkoa na Halmashauri zote
Pololet alisema lengo la chanjo hiyo ni kuwakinga mabinti dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi ambayo inaongoza kwa vifo vya akina mama nchini.
“Wasichana umri wa miaka 14 waliochanjwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi mkoa wa Ruvuma ni 14,786 sawa na asilimia 71 ya lengo la kuchanja wasichana 16,631 sawa na asilimia 80” alisema Pololet
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt.Jairy Khanga alisema changamoto zilizojitokeza wakati wa zoezi hata mkoa kushindwa kufikia lengo la asilimia 80 ni pamoja na imani potofu kwenye baadhi ya maeneo kuwa chanjo hii inaweza kuzuia mabinti kuzaa
Ametaja Halmashauri za Tunduru,Namtumbo na Madaba kufanya vibaya kwenye utoaji wa chanjo hii kutokana na viashiria vya uwepo wa imani potofu kwenye jamii hivyo wasichana kutojitokeza kupata chanjo
Dkt.Khanga alizitaja halmashauri zilizofanya vizuri mwaka huu kuwa ni Mbinga DC (100%) na Nyasa (83%)
“Serikali imeridhia chanjo hii kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 baada ya kufanya utafiti kujiridhisha kutokuwa na madhara kwa watu “ alisema Dkt.Khanga
Dkt.Khanga alitoa wito kwa viongozi wa dini na mila kwenye mkoa wa Ruvuma kusaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo hii kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha ubora wake katika kudhibiti saratani ya mlango wa kizazi.
Kwa mujibu wa Dkt Khanga , vifo 403,000 vilitokea nchini Tanzania kwa mwaka kutokana na saratani ambapo saratani ya mlango wa kizazi kwa akinamama iliachangia asimilia 37.
“Saratani ya shingo ya uzazi Tanzania inaathiri zaidi ya (37%),saratani ya matiti (12%) na saratani ya koo (6.7%) ndio maana serikali ikaja na mkakati wa kuzuia isiendelee “ alisisitiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Katika kikao hicho cha tathmini mkoa uliazimia kuhakikisha unafanya ufuatiliaji wa mabinti waliokwisha chanjwa kujua maendeleo yao na kuhuisha taarifa za halmashauri.
Wito umetolewa pia kwa viongozi wa wilaya kuendelea kuhamasisha wananchi kuhusiana na chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kupitia vyombo vya habari na sanaa katika maeneo yao
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa