MKUU wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amemwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea kupitia kwa maafisa afya kuwapiga faini ya sh. 50,000 kwa kila mwananchi ambaye hatashiriki Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi ambayo ni siku maalum ya kufanya usafi katika maeneo ya umma.Mgema ametoa agizo hilo leo katika Mtaa wa Mwinyi Mkuu Moyo, Kata ya Majengo Manispaa ya Songea ambapo Mkuu huyo ameshirikiana na wananchi wa Mtaa huo kufanya usafi wa Mazingira.
Mgema amesisitiza kuwa sheria ya usafi wa mazingira inawatia hatiani wale wote waliosababisha kuwepo kwa uchafu na wale wanaokataa kufanya usafi wa Mazingira na kwamba adhabu yake ni faini ya sh 50,000 .Amewaagiza watendaji wa mitaa kuwaandika majina wananchi wanaoshiriki usafi wa Mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi na kwamba wale wote ambao hawafiki wapigwe faini ambapo ameagiza Jumatatu ya Oktoba 30 anataka majina ya waliopigwa faini na kiasi cha fedha kilichopatikana kutokana na faini za usafi wa Mazingira.
Mkuu huyo wa wilaya pia amezikumbusha kaya zote katika mitaa 95 ya Manispaa ya Songea kuchangia mchango wa usafi wa Mazingira sh.2000(Elfu mbili) ambao unafanyika kila mwezi.“Usafi wa Mazingira ni jambo la lazima ili kukabiliana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu na malaria’’,anasisitiza Mkuu wa Wilaya.
Amesema katika nchi zilizoendelea hakuna watu wanaougua magonjwa yanayotokana na uchafu na kwamba nchi hizo zinashangaa kuona kuna watu wanaugua na kufa kutokana na magonjwa ya uchafu.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa