Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
28.01.2022
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea limepitisha bajeti ya kiasi cha shilingi Bilion 45,745,490,824 kwa mwaka wa fedha 2022/2023, kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akiwasilisha Rasimu ya mpango na bajeti kwa baraza maalum la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo tarehe 28 Januari 2022, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Dkt. Frederick Sagamiko alisema kuwa maandalizi ya mpango na bajeti ya Halmashauri hiyo umezingatia muongozo wa maandalizi uliotolewa na Wizara ya Fedha na mipango mnamo mwezi Desemba 2021 pamoja na sera na mikakati mbalimbali.
Alibainisha kuwa mpango na bajeti hiyo umezingatia vipaumbele katika maeneo ya kuboresha makusanyo ya mapato ya ndani, kuboresha na kuimarisha huduma za kijamii, kuimarisha utawala bora pamoja kuboresha uratibu, usimamizi, tathimini katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya Manispaa ya Songea.
“Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepanga kukusanya na kutumia kiasi cha Tsh. 45,745,490,824.00 ambapo kati ya fedha hizo matumizi ya mishahara ni sh. 28,982,387,180, matumizi mengineyo ni sh. 1,195,013,000, ruzuku ya miradi ya maendeleo toka Serikali kuu sh. 10,054,548,500 pamoja na fedha kutoka mapato ya ndani sh. 5,634,572,124.” Alibainisha.
Aliongeza kuwa katika mpango na bajeti ya Manispaa kwa mwaka 2022/2023 unalenga kutekeleza ujenzi wa ofisi kuu ya Manispaa, ununuzi wa gari (Mini bus) kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo, ununuzi wa pikipiki kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa kata katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pamoja na kuwezesha mitaa kwa kupeleka sh. 200,000 kila mwezi kwa ajili ya uendeshaji.
Naye, Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano ametoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea pamoja na wataalamu kwa kuandaa bajeti ambayo imegusa kila eneo muhimu kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Songea.
Ametoa rai kwa wataalamu na wasimamizi wa miradi ambayo bado ipo katika utekelezaji kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kabla ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/2023 itakapofika mwezi Julai 2022.’Alisisitiza’
Kwa upande wao Waheshimiwa Madiwani kwa pamoja wamepitisha mpango na bajeti wa Manispaa ya Songea kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na wametoa pongezi kwa wataalamu kwa kuendesha mchakato wa maandalizi ya bajeti hiyo kwa uwazi pamoja na kugusa shughuli za maendeleo kwa wananchi.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa