HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea katika Mkoa wa Ruvuma ni Miongoni mwa Halmashauri za miji 18 nchini inayotekeleza Mradi wa uendelezaji Miji na Manispaa unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.
Mchumi Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Raphael Kimary anasema Manispaa hiyo imepanga kutekeleza miradi nane chini ya mradi wa uendelezaji Miji na Manispaa katika Kipindi cha Kuanzia mwaka wa Fedha wa 2017/2018.
Kwa mujibu wa Kimary,Manispaa ya Songea inatarajia kutumia zaidi ya sh.bilioni 21.8 katika kutekeleza miradi hiyo ambayo inatekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Anaitaja miradi hiyo kuwa ni Miradi ukarabati barabara kwa kiwango cha lami km 10.3 kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 10 na ujenzi wa Stendi Mpya ya mabasi katika eneo la shule ya Tanga kwa gharama ya sh. bilioni sita.
Miradi mingine ni ujenzi wa Machinjio ya kisasa zaidi ya sh. bilioni tatu,ukarabati wa dampo sh. bilioni 1.5,Kujenga uwezo watumishi na viongozi wa kisiasa sh. milioni 200 na ukarabati wa bustani ya Manispaa sh.milioni 399.
Jambo la kutia moyo ni kwamba Halmashauri ya Manispaa ya Songea tayari imepokea fedha za awali kwa ajili ya kutekeleza program ya uboreshaji wa Miji na Manispaa(ULGSP) inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na kwamba baadhi ya miradi imekamilika.
Hata hivyo anasema mradi umedhamiria kuongeza mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa mapato,kuimarisha uzingatiaji wa sheria,kanuni na miongozo ya serikali,ujenzi wa miundombinu, kuongeza,uwajibikaji,usimamizi wa rasilimali za Halmashauri na kujenga uwezo wa Halmashauri.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Abdul Hassan Mshaweji anasema Manispaa hiyo imeweka mpango mkakati wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2019/2020 ili kuwa na mwelekeo wa utoaji wa huduma za msingi za kuanzishwa kwa Halmashauri ya jiji la Songea.
Mshaweji anabainisha zaidi kuwa manispaa inatarajia kufikia malengo ya kuwa jiji kwa kuzingatia Sayansi, teknolojia, utawandawazi na soko huru kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu na kuongeza ufanisi mkubwa kwa kutumia utawala bora ili kuinua na kuboresha maisha ya wakazi wa manispaa hiyo.
Ili kuhakikisha uchumi wa Halmashauri ya Manispaa unakua,Mshaweji ameutaja mwelekeo ni kuongeza uzalishaji na mauzo ya bidhaa, kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki pamoja na kuwa na miradi ya uzalishaji yenye tija na utendaji wenye maadili na nidhamu kwa kuzingatia kauli mbiu ya Hapa kazi tu ifikapo mwaka 2017.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jimbo moja la Uchaguzi,tarafa mbili ambazo ni tarafa ya Mashariki na tarafa ya Magharibi, ina kata 21 na Mitaa 95,yenye jumla ya Kaya 61,930.
Manispaa hiyo inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 237,843 wakiwemo Wanaume 112,420 na Wanawake 125,423 ambalo ni ongezeko la asilimia 4.4 kwa mwaka.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 16,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa