Na; Amina Pilly – Songea Mc
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali . Ahmed Abbas Ahmed ameshiriki makabidhiano ya Mkataba kwa mkandarasi wa ujenzi wa masoko ya kisasa ya Manzese A & B pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka yakijumuisha jumla ya Bil. 22.9.
Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma walioshiriki mkutano huo ametoa wito kwa Mkurugenzio wa Halmashauri hiyo wakati wa kutekeleza mradi huo ni muhimu kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa eneo hilo.
Kanali Abbas amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwakuwa ametambua umuhimu wa wataalamu ambao wamechagiza na kuweka sawa hatua mbalimbali za awali za maandalizi ya soko hilo wasipongezwe kwa maneno ni muhimu wapewe zawadi ambayo ataona inafaa, ambapo miongoni mwa Idara zilizoshiriki katika kufanikisha mradi huo ni idara ya ujenzi, manunuzi, pamoja na TARURA.
Ametoa wito kwa Mkandarasi kuhakikisha anasimamia na kutekeleza vizuri mradi huo na kuhakikisha anaajiri wazawa ili kuendana na maombi ya mwenyekiti wa mtaa wa Majimaji ambayo yamewasilishwa wakati akifungua kikao hicho.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa mtaa wa Majimaji alisema wananchi wa mtaa huo wameupokea mradi huo vizuri na watatoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi ikiwemo na kuhakikisha ulinzi na usalama wa mradi huo.
Akizungumza Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Wakili Bashir Muhoja alisema, Mradi wa TACTIC (Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness Project) ni mojawapo ya miradi inayotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais -TAMISEMI kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia ambao unalenga kuboresha miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania Bara pamoja na kujengea uwezo wa Taasisi kwenye Halmashauri husika ili ziweze kujiimarisha katika usimamizi wa uendelezaji Miji pamoja na ukusanyaji wa mapato.
Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni miongoni mwa Miji 45 ambayo imepewa kipaumbele cha kupata ufadhili wa mradi huu wa uboreshaji miundombinu ya Miji, Manispaa na Majiji ambapo Mradi huu unatekelezwa kwa awamu mbili katika Manispaa ya Songea ikiwa awamu ya kwanza ni ya ujenzi wa barabara za Mjini zenye jumla ya Kilometa 10.01 ambapo hadi kukamilika utagharmu jumla ya Shilingi 22,274,733,277.02 uko katika hatua ya ukamilishaji.
Awamu ya pili (Package 2) ni ya ujenzi wa Miundombinu ya Ujenzi wa soko la Manzese A na Ujenzi wa Soko la Manzese B pamoja na Ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mazao ya kilimo (agro-processing Industry) katika eneo la Lilambo.
Aidha, Katika hatua ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi huu ni pamoja na Usanifu wa mradi uliofanyika kuanzia Mei, 2022 hadi Februari, 2023 ambapo Zabuni za kutafuta Wakandarasi zilitangazwa mwezi Machi, 2025 na kukamilika Julai 2025.
Aliongeza kuwa Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi: M/S China National Aero Technology International Engineering Corporation kwa gharama ya shilingi 22,914,943,624.67 chini ya Mhandisi Mshauri: M/S Howard Consulting LTD kwa gharama za shilingi 938,395,000.00 ambapo gharama hii ya Mhandisi Mshauri inajumuisha usimamizi wa mradi wa ujenzi wa barabara, masoko na kiwanda.
Alisema Miundombinu itakayojengwa katika Masoko ya Manzese A na B na Kiwanda cha kuchakata Mazao ni pamoja na; Maduka 310, maduka 20 ya huduma ndogo za kibenki, vyumba vya vyoo 43, Vizimba 1628, Baa 6, Ghuba 4 za kukusanyia taka, Baa ya kienyeji moja (1), Maeneo 3 ya kutoa faragha ya kunyonyesha/kulea watoto wadogo na eneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) 354 (eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 708).
Aidha, Kwa upande wa Kiwanda cha kuchakata Mazao, miundombinu inayotegemewa kujengwa ni maghala nane, Jengo la Utawala, Jengo la uchakataji Mazao ya nafaka, Jengo la mama lishe, Jengo la Ofisi ya Mawakala, Vyoo, Ofisi ya mizani na ghuba la kukukusanyia taka.
Muhoja aliongeza kuwa Mandalizi ya Utekelezaji wa Mkataba wa ujenzi wa Masoko ya Manzese A na B pamoja na Kiwanda cha uchakataji mazao unatarajiwa kuanza tarehe 15/07/2025 na kumalizika 15 Julai 2026 kwa mujibu wa Mkataba uliosainiwa rasmi tarehe 25 Juni, 2025.
Mradi wa ujenzi wa masoko na Kiwanda cha usindikaji mazao unatarajia kuleta manufaa ya Kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara katika shughuli zao, Kutoa ajira za moja kwa moja kwa Wananchi watakaofanya biashara katika maeneo ya masoko na kiwanda, Kuongeza thamani ya mazao na kuwezesha wananchi/wakulima na kuongeza kipato kwa wakulima na wafanyabiashara, Kuongeza makusanyo ya Halmashauri ambapo jumla ya shilingi 1,062,000,000.00 zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka.
“Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Menejimenti, Watumishi na Wananchi wote kwa ujumla tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dr. Samia Suluhu Hassan Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amewezesha upatikanaji wa fedha za Mradi huu mkubwa kabisa.
Mkabidhiano hayo yamefanyika tarehe 05 Julai 2025 katika viwanja vya eneo la mradi wa ujenzi wa soko la Manzese A ambayo yalihudhuriwa na wananchi mbalimbali, viongozi ngazi ya mkoa, Wilaya, Kta, Mitaa pamoja na Wahandisi watakaosimamia mradi huo.
MWISHO.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa