Halmashauri ya Manispaa ya Songea imefanya bonanza la michezo siku ya jana tarehe 22 Julai 2021 katika uwanja wa Zimanimoto uliopo katika Manispaa ya Songea ikiwa ni utekelezaji wa kauli iliyotolewa na Mheshimiwa Innocent Bashungwa Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo kwamba “Watumishi wote kujijengea tabia ya kufanya mazoezi baada ya masaa ya kazi kwa lengo la kuimarisha afya, burudani pamoja na kujenga mahusiano mazuri baina ya watumishi kazini”.
Bonanza hilo lilifanyika kwa kucheza michezo kati ya Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Songea na wafanyakazi waliopo ofisi kuu Manispaa ya Songea ambapo miongoni mwa michezo iliyofanyika ni pamoja na mchezo wa mpira wa miguu uliochezwa kati ya timu ya Waheshimiwa Madiwani na timu ya wataalamu Manispaa ya Songea, na kumalizika kwa mchezo kwa sare ya magoli 2-2.
Katika mchezo huo timu ya Waheshimiwa Madiwani walianza kwa kufunga goli la kwanza ndani ya dakika 15 goli lililofungwa na Mheshimiwa diwani kutoka kata ya Bombambili Jeremiah Mlembe (Naibu Meya), na hatimaye kusawazisha goli hilo na mchezaji Salingwa Elias kutoka timu ya wataalamu Manispaa ya Songea, Hadi kufika kipindi cha mapumziko timu zote mbili zilipata ushindi wa goli mojamoja.
Baada ya mapumziko timu zote mbili zilitinga uwanjani kwa kujiamini kila mmoja kuwa mshindi, pia dakika 69 kipindi cha pili timu ya Waheshimiwa Madiwani walitikisa nyavu za timu ya wataalamu kutoka Manispaa na kufunga goli la pili, goli ambalo lilifungwa na Mheshimiwa Diwani kutoka kata ya Lizaboni Oddo Mbunda, huku mashambulizi yaliyorejeshwa na Kongolo Fossi mchezaji kutoka timu ya wataalamu kwa kufunga goli la pili katika dakika ya 86.
Kwa upande wa mchezo wa mpira wa kikapu kwa wanawake kati ya timu ya Waheshimiwa Madiwani na timu ya Wataalamu Manispaa ulimalizika kwa ushindi wa kishindo ambapo timu ya wataalamu Manispaa walioongoza kwa magoli 22 huku timu ya Waheshimiwa Madiwani ikipata magoli 6.
Nae Mheshimiwa Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano amesema kwamba amefurahishwa sana uandaaji wa bonanza hilo na ameeleza kuwa matarajio yake ni kuona bonanza hilo la michezo linaendelea kufanyika kila mwishoni mwa mwezi. ’Alisisitiza’.
Bonanza hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo pamoja na wakuu wa Idara mbalimbali ndani ya Manispaa ya Songea pamoja na wananchi.
IMEANDALIWA NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
23.07.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa