Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi kampeni zake za kuwanadi wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kwa Mkoa wa Ruvuma, kupitia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika tarehe 15 Septemba 2025 katika viwanja vya Shule ya Msingi Namtumbo.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Mhe. Ally Salum Hapi, pamoja na maelfu ya wanachama na wapenzi wa CCM. Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kufungua rasmi kampeni kwa ajili ya kuwanadi wagombea wote wa CCM kupitia nafasi za ubunge na udiwani katika Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Hapi aliwashukuru wananchi na wapenzi wa CCM kwa kujitokeza kwa wingi, huku akiwapongeza kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Aidha, alieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Samia, hususan katika sekta za afya, elimu, miundombinu, na uwezeshaji wa wajasiriamali.
Mhe. Hapi alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanachama na wapenzi wa CCM kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nafasi ya urais kupitia CCM, akisisitiza kuwa bado yapo mengi makubwa atakayoyafanya kwa maendeleo ya Taifa na hasa kwa Mkoa wa Ruvuma ambapo aliongeza kuwa zaidi ya Tsh bilioni 200 zimetengwa kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali, pamoja na maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za afya.
Aidha, aliwahimiza wanachama na wananchi wote kuwapigia kura wagombea wa CCM katika nafasi za ubunge na udiwani ili kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi ujao.
Katika mkutano huo wa hadhara, walihudhuria pia wagombea mbalimbali wa nafasi ya ubunge na udiwani akiwemo:
Dkt. Juma Omera – Mgombea ubunge Jimbo la Namtumbo
Dkt. Damas Ndumbaro – Mgombea ubunge Jimbo la Songea Mjini
Mhe. Jenister Mhagama – Mgombea ubunge Jimbo la Peramiho
Jackline Msongozi na Mariam Nyoka – Wagombea wa ubunge viti maalum Mkoa wa Ruvuma
Akizungumza mgombea wa jimbo la Namtumbo Dkt. Juma Homera ambaye alisema anafahamu wananchi wa wanamtumbo wanahitaji kuboreshewa na kupata huduma za maji, Barabara, Afya pamoja, elimu, kilimo pamoja na huduma mbalimbali kwa wananchi, na baada ya kusema hayo aliomba kura kwa wananchi.
Mkutano huo ulihitimishwa kwa hamasa kubwa kutoka kwa wanachama na wapenzi wa CCM, huku wakiahidi kuiunga mkono CCM kwa ushindi mnono katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa