MAFUNZO ya utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi yalioshirikisha walimu wa afya na wahudumu wa Afya ya msingi Zaidi ya 300 kutoka katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma yamefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa hiyo mjini Songea.
Mafunzo hayo yamefanyika kabla ya Jumatatu Aprili 23 mwaka huu siku ambayo utafanyika uzinduzi wa Mkoa wa Ruvuma wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14.
Uzinduzi wa chanjo hiyo kimkoa unatarajiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea,Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo Dk.Mameritha Basike amelitaja lengo la Manispaa hiyo ni kutoa chanjo ya mlango wa kizazi kwa wasichana 1834 ambapo lengo la Mkoa wa Ruvuma ni kutoa chanjo hiyo kwa wasichana 28,676.
“Manispaa ya Songea tumejipanga kuhakikisha kuwa tunatoa chanjo hiyo kwa asilimia kati ya 99 hadi 100,zoezi hili katika mkoa wetu litaanza Aprili 23 hadi 29,baada ya hapo zoezi hili la utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi litakuwa endelevu’’,anasisitiza Dk.Basike.
Kwa mujibu wa Dk.Basike, chanjo hiyo ni muhimu kwa sababu itapambana na virusi vinavyoitwa Human Papiloma Virus(HPV) ambavyo huambukizwa kwa njia ya ngono na kwamba chanjo inakusudia kuweka kinga dhidi ya kirusi hicho ambacho kinasababishwa na kufanya ngono katika umri mdogo.
Mmoja wa watoa mada katika mafunzo hayo Flowin Komba amevitaja visababishi vya saratani ya mlango wa kizazi kuwa ni kuanza ngono katika umri mdogo,kufanya ngono na wapenzi wengi,historia ya kubeba mimba nyingi na uvutaji wa sigara,tumbaku na ugoro.
Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka wagonjwa 6000 wa saratani za mlango wa kizazi na matiti wanagundulika kati yao wagonjwa 4000 wanapoteza maisha.
Takwimu za Taasisi ya saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa mwaka 2015 Tanzania ilikuwa na wagonjwa wa saratani 2500 ambapo mwaka 2015 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 5200 sawa na ongezeka la asilimia 100.
Kulingana na takwimu za Ocean Road,saratani za mlango wa kizazi na matiti husababisha asilimia 50 ya vifo vyote vinavyotokana na saratani kwa akinamama na kwamba kila watu 100 wanaochunguzwa,wanabainika wagonjwa 36 kuwa na saratani.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Aprili 21,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa