TANZANIA inatarajia kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa chuma katika Bara la Afrika kwa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka pindi uzalishaji wa madini hayo utakapoanza katika eneo la Liganga Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe.
Meneja Uhusiano wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Abel Ngapemba anasema mradi huo wa uzalishaji chuma utatekelezwa chini ya Kampuni ya Tanzania China Mineral Resources Limited (TCIMRL),
Hata hivyo anasema kampuni hiyo ni ya ubia kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Shirika la Sichuan Hongda Group (SHG) ya China utaenda sanjari na uzalishaji wa madini ya Titanium na Vanadium.
Mradi huo ukikamilika tutaweza kuzalisha tani milioni 219 za chuma ambazo zitadumu kwa zaidi ya miaka 70, na madini mengine yatakayotokana na mgodi huo ni Titanium tani 175,400 kwa mwaka na Vanadium tani 5,000 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa Ngapemba uzalishaji huo utaiwezesha Tanzania kushika nafasi ya nne kwa uzalishaji wa chuma ikizifuatia nchi ya Afrika Kusini inayozalisha bidhaa za chuma tani milioni 8.5 kwa mwaka, Misri tani milioni 8.0 na Libya tani milioni 2.0 kwa mwaka.
Mradi huu ni moja ya miradi miwili iliyopo katika mkataba kati ya NDC na SHG uliotiwa saini Septemba 2011 ya uanzishwaji wa mgodi wa mkaa wa mawe na ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa megawati 600 katika eneo la Mchuchuma.
Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovoti 220 kati ya Mchumchuma na Liganga, na uanzishwaji wa mgodi wa chuma pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua chuma , kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma na ujenzi wa barabara kati ya Mchuchuma na Liganga.
Chuma kinachozalishwa duniani ni takribani tani bilioni 1.55 kwa mwaka, mzalishaji mkubwa ikiwa ni China inayotoa tani milioni 711 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 46 ya chuma chote kinachozalishwa duniani.
Miradi hii itakayogharimu Dola za Marekani bilioni 3 inatarajiwa kuliingizia Taifa mapato ya dola bilioni 1.7 kwa mwaka itakapoanza uzalishaji wake.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa