WIZARA ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kupitia kitengo cha mawasiliano serikali imeongoza jopo la wanahabari toka vyombo mbalimbali nchini ambao wametembelea shule ya msingi Tembo Mashujaa iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Wanahabari toka jijini Dar es salaam wa luninga,magazeti,redio na mitandao ya kihabari,wakiwa katika shule hiyo walimshangaa mwalimu Asumpta Banda ambaye anafundisha darasa la kwanza linaloongea lenye wanafunzi 146 ambao wote wanajua kusoma,kuandika na kuhesabu(KKK).
Kwa mujibu wa Mwalimu Banda darasa linaloongea linamwezesha wanafunzi wake wanaosoma darasa la kwanza kujua (KKK) katika kipindi cha miezi mitatu.
Afisa Elimu Msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Consesa Mbena amesema shule zote za msingi katika Manispaa hiyo kwa madarasa ya kwanza hadi la tatu yana madarasa yanayoongea.
Hata hivyo amesema shule zinaoongoza kwa kuwa na madarasa bora yanayoongea ni shule ya msingi Tembomashujaa,Kambarage na Mashujaa.
“Mwalimu Asumpta Banda katika shule ya msingi Tembo Mashujaa,amekuwa anafanya vizuri katika darasa linaloongea, walimu wengine katika Manispaa yetu wamekuwa wanakwenda kujifunza kwake,mwalimu huyu anastaafu Novemba mwaka huu’’,anasema Mbena.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imedhamiria kuleta Mapinduzi ya Kielimu ambapo kila shule ya msingi nchini inatekeleza mtaala mpya wa kuwa na darasa la KKK ambalo linaongea.
Darasa linaloongea limeandaliwa kwa kuwekwa zana za kufundishia na kujifunzia ambazo zina Uwezo wa kumshawishi Mtoto kutaka kujifunza Zaidi bila hata ya uwepo wa mwalimu darasani.Faida kubwa ya Darasa linaloongea ni kupunguza idadi kubwa ya utoro shuleni,mwanafunzi kuwa mdadisi,mwanafunzi kuwa mbunifu,kuleta ari ya kujifunza kwa mwanafunzi na kupunguza kelele darasani.
Iwapo kila shule ya msingi nchini itakuwa na darasa linaloongea lenye zana za kutosha,zinazoonekana na kusomeka Vizuri, idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu nchini itapungua na kumalizika.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 19,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa