Ugonjwa wa Usubi ni miongoni mwa magonjwa yaliyopo katika kundi la magonjwa yasiyopewa kipaumbele sana katika jamii ikiwemo na ugonjwa wa matende na mabusha, kichocho, kikope, pamoja na minyoo ya tumbo.
“Kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika hali ya uwepo wa magonjwa haya katika Manispaa ya Songea imepungua kwa kiasi kikubwa ambapo hasa ugonjwa wa matende na mabusha na hivyo nguvu kubwa inawekezwa katika kuuthibiti ugonjwa wa usubi pamoja na minyoo ya tumbo” hayo yamebainishwa na Mratibu wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele Manispaa ya Songea Broad Komba wakati akizungumza na watendaji wa kata zote 21 pamoja na wenyeviti wa mitaa 95 katika ukumbi wa Manispaa ya Songea leo tarehe 24 Agosti 2021 kwa lengo la kuwapa elimu ili kurahisisha zoezi la ugawaji wa dawa kinga za ugonjwa wa Usubi.
Komba amesema kuwa katika kipindi kilichopita walifanikiwa kwa asilimia 97% kugawa dawa za minyoo ya tumbo kwa wanafunzi wote wa shule za msingi Manispaa ya Songea na hivyo wamejipanga katika awamu ya pili kugawa dawa za ugonjwa wa usubi kwa kaya zote zilizopo ndani ya Manispaa ya Songea.
Amewataka viongozi hao wa kata na mitaa kwenda kuwahamasisha wananchi juu ya kutumia dawa kinga hizo za usubi ili kuweza kupunguza madhara yatokanayo na ugonjwa huo ambapo zoezi linatarajiwa kuanza tarehe 27 hadi 29 Agosti 2021 na wamekadiria kutoa dawa hizo kwa wananchi wote ’Alibainisha’.
Komba alihitimisha kwa kuwasisitiza wenyeviti wa mitaa kuhakikisha watu wanaowachagua kugawa dawa hizo wawe wanatoka katika maeneo husika, lazima ajue kusoma na kuandika, awe ana uzoefu wa kujitolea kwenye sekta ya afya pamoja na kuzingatia makundi maalumu ambayo hayatakiwi kutumia dawa hizo ambao ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wakinamama wajawazito.
Naye mganga mkuu wa Manispaa ya Songea Amosi Mwenda ametoa rai kwa viongozi hao kuendelea kutoa elimu kwenye maeneo yao juu ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya ugonjwa huo ambayo inatolewa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, kituo cha afya Mjimwema na kituo cha afya Mshangano.
NA AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA,
24.08.2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa