Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yalianza karne ya 18 wakati wa mapinduzi ya viwanda yanashika hatamu Barani Ulaya hususani katika Taifa la Uingereza ambayo huamdhimishwa Dunia kote, na kwa mwaka 2021 Mkoa wa Ruvuma imeadhimisha sherehe hizo Wilayani Nyasa katika uwanja wa Fisheries.
Kutokana na uchache wa watendaji kazi na tamaa za Wajiri kwa wakati huo kutaka kuzalisha Zaidi kwa faida Zaidi, Wafanyakazi walifanya kazi masaa 18 mfululizo na kwa ujira mdogo ambapo hali hiyo ilipelekea kuanzishwa kwa vuguvugu la mapinduzi ya kujinasua na ukandamizaji wa waajiri, na kushinikiza muda wa kazi upungue hadi kufikia masaa 9.
Sheria ya vyama ya ajira na mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004 imeeleza wazi uwepo wa vyama vya wafanyakazi ni miongoni mwa msingi wa haki za wafanyakazi popote duniani.
Risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Mkoa wa Ruvuma (TUCTA) iliyosomwa Mkutanoni hapo ambayo ilisema “lengo la maadhimisho hayo ni kukumbuka wafanyakazi waliojitokeza kupinga unyanyasaji, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa na mabepari huko Ulaya katika kipindi cha Mapinduzi ya viwanda na Mapinduzi ya kilimo katika karne 18”.
TUCTA waliongeza kuwa ni ukweli usiopingika mishahara ya wafanyakazi kwa Taifa letu ni midogo ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha hivyo kupitia maadhimisho hayo waliiomba Serikali kupandisha madaraja ya mishahara kwa watumishi, na kulipa madeni mabalimbali ya watumishi.
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili watumishi ni pamoja na baadhi ya watumishi kutolipwa madeni yao ya uhamisho wanapohama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, watumishi kutopandishwa madaraja kwa muda mrefu, baadhi ya waajiri kushindwa kufanya mabaraza ya wafanyakazi jambo ambalo linawanyima haki wafanyakazi haki ya ushirikishwaji, kufanyishwa kazi siku ya mapumziko na Baadhi ya waajiri hususani Sekta binafsi kukiuka sheria za wafanyakazi ya kuwafanyisha kazi watumishi na kutowalipa mishahara watumishi kwa wakati pamoja na kutotoa mikataba ya ajira. “TUCTA walibainisha”.
Sambamba na changamoto mbalimbali TUCTA wameahidi kufanya kazi kwa bidii zao zote kwa maslahi mapana ya Nchi na Mkoa wa Ruvuma wakiamini Serikali itachukua hatua za dhati kutatua changamoto na kuondoa malalamiko ya watumishi.
TUCTA wametoa Rai kwa wafanyakazi wote Mkoani Ruvuma kujihadhari na maambukizi ya Virus vya Ukimwi kwani ni ugonjwa hatari kwa Taifa letu.
TUCTA wamekemea vikali watumishi wasiowajibika, wabadhilifu wa mali za mwajiri, wazembe kazini, wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kazini kuwa vitendo hivyo havikubaliki katika utumishi wa umma na mahala popote.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ambaye amepata uteuzi hivi karibuni kuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Taifa ambapo alisema “kuhusu mishahara kuweni na subira kwani Serikali ya awamu ya sita imedhamilia kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuanza kupandisha madaraja kwa wale wanaostahili na kuhakikisha mtumishi anapanda cheo pamoja na kujali maslahi ya wafanyakazi.”
Chilumba amewataka waajiri kuhakiki madeni yote ya watumishi na kuhakikisha watumishi wastaafu wanalipwa madeni yao, Waajiri wanatakiwa kushirikisha mabaraza ya wafanyakazi ikiwa ni moja ya nguzo ya ushirikishwaji, Waajiri wote wanatakiwa kuunda mabaraza ya wafanyakazi, na taasisi zote Serikali zenye madeni ya watumishi zitumie fedha zake za ndani kulipa madeni pamoja na kutenda haki kwa watumishi kwani kutofanya hivyo ni kuwavunja moyo watumishi walio chini yao. “Alisisitiza”.
Aliongeza kuwa, pamoja na kuendelea kudai maslahi juu, mshahara juu, lakini itimizwe wajibu.
Alisema Serikali Mkoani Ruvuma haitavumilia kuendelea kupokea malalamiko ya watumishi ambao hufanyishwa kazi nje ya mkataba, kuachishwa kazi nje ya utaratibu, kulipa kiwango kisicho stahili, kuchelewa kulipa mishahara ya watumishi kwani kufanya hivyo ni kuvunja haki za binadamu na kukiuka sheria ya Nchi ya Tanzania.
Kauli mbiu ya mwaka 2021; Maslahi bora, Mishahara juu, Kazi iendelee.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
02 MAY 2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa