YEYOTE atakaye amua kufunga biashara yake hatumlazimishi kwasababu hata wakati anafungua aliamua yeye mwenyewe kwa hiyo hata akiamua kufunga afunge.
Hayo yamebainika katika kikao cha baraza la madiwani Manispaa ya Songea kilichohudhuriwa na Mh Mbunge jimbo la Songea Mjini Dr Damas Ndumbaro Waziri wa Maliasili na Utalii, wananchi mbalimbali, wataalamu, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea tarehe 17 februari 2021.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza la Madiwani Manispaa ya Songea alisema vikao vya baraza la madiwani vipo kwa mujibu wa sheria na hufanyika kila robo moja ya mwaka kwa ajili ya kujadili maendeleo ya halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Mbano alisema Halmashauri imejipanga katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo ikiwa ni hatua ya kuanza utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kuweka mpango na bajeti rafiki wenye sura ya utekelezaji wa Ilani ambao utapitishwa kupitia vikao vya Halmashauri.
Naye naibu meya Manispaa ya Songea jeremia Milembe akitoa ufafanuzi juu ya matumizi sahihi ya kituo cha mabasi Songea alisema nanukuu“ tuliamua wenyewe kwenye baraza hili juu ya matumizi sahihi ya stendi ya Tanga, tushikamane kwa pamoja katika jambo hili, lakini kuna baadhi ya Madiwani wanatumika na wafanyabiashara ‘ huo ndiyo ukweli” mwisho wa kunukuu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema akihutubia Baraza hilo la madiwani ambapo alianza kwa kusema mapato ya ndani ya Halmashauri husika mna mamlaka ya kuyaelekeza katika vipaumbele vyenu ambavyo ni vya umuhimu kwa wakati huo ambapo katika kutekeleza Elimu bure mmekutana na ongezeko kubwa la watoto shuleni kwa hiyo miundombinu ya kutolea Elimu hiyo yataendelea kuwa na upungufu.
Pololet amewataka Wataalamu hao kutenga bajeti kwa ajili ya kusaidia kukamilisha majengo yaliyoanzishwa na wananchi pamoja na kushughulikia changamoto za miundombinu ya shule haraka iwezekanavyo kabla ya tarehe 28 februari 2021 ambapo kila Halmashauri inatakiwa itoe taarifa za utekelezaji wa agizo hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kituo kikuu cha mabasi Songea ambapo alianza kwa kusema “ udiwani sio kazi, na kama huna kazi usigombee udiwani kwahiyo wanaofanya biashara maana yake wanakazi na wanastahili kupata udiwani. Sasa usichanganye (CONFLICT INTEREST) tumia vizuri sana nafasi yako ya uwakilishi kwa wananchi usiende kuharibu maslahi ya walio wengi.”
Alisema kunachangamoto ya kuwa na uongozi wa wafanyabiashara ambao huchukua mambo yao binafsi na kuhamasisha wafanyabiashara wenzake waunge mkono mambo ambayo yanamuhusu yeye mwenyewe.
Aliongeza kuwa wapo wafanyabiashara ambao wanafanya biashara bila kulipa kodi na wengine hawatoi risiti ya EFD- Electronic Fiscal Device, na baada ya kuwabaini walilipa faini/adhabu kutokana na tukio hilo, walikaa kikao na kusema Serikali inakusanya kodi kwa kutumia polisi ‘hiyo siyo kweli ‘. Pololet alikanusha.
Alisema polisi walikuwa wanafanya kampeni ya kukamata wamiliki wa nyumba za kulala wageni ambao hawajarasimisha biashara zao ( maarufu kama GUEST BUBU ) ambazo zinatumika vibaya kuficha watu ambao wanaviashiria vya uhalifu na baada ya kuwakamata walilipa adhabu pamoja na kurasimisha biashara zao. Moja ya kazi ya jeshi la Polisi ni kuhakikisha jamii inakuwa salama. Hata hivyo baada ya tukio hilo, wamechukia na kuchanganya makosa yao na kuanza kusema Serikali inakusanya kodi kwa kutumia polisi.
Amewataka madiwani hao kuacha kujihusisha kwenye migomo ya wafanyabiashara na ikiwezekana kuacha kuingia kwenye vikao vya wafanyabiashara hao sababu migomo hiyo ni haramu na mkiendelea mtachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mh Mbunge Jimbo la Songea Mjini Dr Damas Ndumbaro Waziri wa Maliasili na Utalii alisema tuliamua sisi wenyewe kupeleka Stendi Tanga. Jambo la msingi ni kupunguza maumivu kwa pale inapohitajika kwa kutumia vituo mbalimbali kama Ruhuwiko, Seedfarm,na Bombambili.
Dr Ndumbaro alibainisha kuwa atakuwa na ziara ya kuzungukia kata zote 21 zilizopo manispaa ya Songea kwa lengo la kutoa shukrani kwa wananchi ambapo katika ziara hiyo atazungumzia zoezi la upandaji miti ambalo litafanyika kata zote 21 za Manispaa ya Songea, ufugaji wa nyuki, pamoja na uhamasishaji wa utalii wa ndani.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
18/02/2021.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa