Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba amewataka wanaume kuwa majasiri wa kupima afya zao badala ya kutegemea majibu ya wenza wao ambao hupima virusi vya UKIMWI kwa lazima wakiwa wajawazito.
Ameyasema hayo wakati akizindua kampeni ya pima jitambue ishi kwa furaha Kiwilaya iliyofanyika jana katika Kijiji cha Litumbakuhamba kata ya Linga Wilayani hapa yenye lengo la kuwahamasisha wanaume kupima afya zao na kujitambua kama wameambukizwa virusi vya UKIMWI ili waweze kuanza kutumia vidonge vya kufubaza virusi vya UKIMWI na ambao hawajaathirika kuchukua tahadhari.
Mkuu wa Wilaya alifafanua kuwa wanaume wengi ni waoga kwenda kupima na kujua afya zao na wanategemea majibu ya wenza wao wakishapima huwauliza vipi majibu mke wake akisema sina maambukizi na mwanaume naye husema hana maambukizi lakini kama mke wake akiwa na maambukizi naye huomba vidonge na kuanza kumeza na huona aibu kwenda kuchukua dawa na hujikuta dozi ya mkewe hugawana wote hali inayoweza kuleta usumbufu miongoni mwao kwa kuwa dawa hizo hutolewa kwa kdozi ya kila mgonjwa.
Aliongeza kusema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kila mwanamke na mwanaume wanapima virusi vya UKIMWI na kujitambua ili waweze kuishi wakiwa na uhakika wa afya zao na wachukue hatua ya kuanza dawa mara baada ya kugundulika wameambukizwa na kwa wale ambao hawajambukizwa wachukue taadhari ya kutunza afya zao.
“Katika maisha tunaamini kuwa wanaume ni majasiri si ndio jamani,lakini kwa siku ya leo napenda kuwaambia kuwa hakuna watu waoga kama hawa wanaume katika kupima virusi vya UKIMWI.Wengi wao wanategemea majibu ya wake zao ili waweze kujua afya zao,lakini kitendo hicho sio kweli kwa kuwa kila mtu anakuwa na afya yake na mwenendo wake.kuna wakati mke ni anakuwa ameathirika na mwanaume ni mzima na wakati mwingine mume kaathirika na mke anakuwa hana maambukizi hivyo ni wajibu wa kila mtu kujua afya yake ili aweze kuishi kwa furaha”.
Wananchi waliokuwepo walifurahia kuhamasishwa huko na wakasema wataendelea kupima afya zao ili waweze kujitambua na kutoa ahadi kwa mkuu huyo watakuwa wanaenda kupima na kujua hali zao za afya.
Awali akitoa taarifa ya upimaji wa virusi vya UKIMWI wilayani Nyasa Kaimu Mganga Mkuu Dkt Aron Hyera alisema mwamko wa upimaji wa virusi vya UKIMWI unaendelea vizuri watu wengi wanahamasika kupima na kwa mwaka huu jumla ya wanaume 79599 sawa na asilimia 56 walipima na kujua afya zao na akinamama 32139 sawa na asilimia 44 walipima afya zao katika Wilaya ya Nyasa.
Katika hatua nyingine Wananchi hao wa kijiji cha Litumbakuhamba waliomba zahanati yao iboreshwe iweze kutoa huduma ya dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kwa kuwa kwa sasa wanapata shida ya kwenda kupata huduma hiyo katika kata ya lituhi ambako ni mbali kutoka katika kijiji Hicho.
IMEANDALIWA NA
NETHO SICHALI
KAIMU AFISA HABARI
NYASA DC
0767417597/0783662568
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa