Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa Jimson Mhagama amebadilisha eneo la kufanyia mikutano ya wakuu wa idara inayofanyika Ofisini kwake kila ijumaa na Jumatatu asubuhi na kufanyia eneo la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa inayojengwa katika Kijiji cha Nangombo Kata ya Kilosa Wilayani hapa ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kabla ya juni 30 mwaka huu.
Ameyasema hayo leo wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya inayoendelea kujengwa katika Kijiji cha Nangombo.
Mhagama alifafanua kuwa amelazimika kubadili eneo la kufanyia vikao vya wakuu wa Idara Wilayani hapa kutoka Ofisini kwake hadi kufanyia eneo la Ujenzi wa Hospitali katika kijiji cha Nangombo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi ili kila mkuu wa idara aone kwa macho maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mpaka itakapokamilika yenye lengo la kutatua kero za wananchi wa Wilaya ya Nyasa waliokuwa wakitembeai umbali wa kilomita 66 kufuata Huduma za Matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya mbinga.
Aliongeza kuwa vikao vyote vya wakuu wa idara alivyokuwa akivifanya Ofisini kwake sasa amevihamishia katika eneo la ujenzi na kila mkuu wa idara na Vitengo wanatakiwa kushiriki bila kukosa mpaka juni 30 tutakapokuwa tumeshakamilisha ujenzi huu wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa.
“kuanzia leo vikao vyote vya kiutawala vinavyojumisha Wakuu wa idara na Vitengo vitakuwa vinafanyika katika eneo la Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyasa katika Kijiji cha Nangombo kata ya kilosa na kila Mkuu wa idara na Vitengo wanatakiwa kufika bila kukosa wala kuchelewa. Mheshimiwa Rais amezitoa fedha hizi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huu kwa wakati tuna kila sababu ya kusimamia ujenzi huu kwa nguvu zote” alisema Mhagama.
Aidha katika hatua nyingine amempongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuwajali wananchi wa Wilaya ya Nyasa kwa kuwapa fedha ya kujengea Hospitali ya Wilaya ya Nyasa kwa kuwa walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Aidha bwana Jimson Mhagama alitoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa kutembelea na kuona jinsi ujenzi unavyoendelea na kutoa maoni na ushauri kwa kuwa Hospitali hii ni mali ya wana Nyasa.
Imeandaliwa na
NETHO SICHALI
AFISA HABARI
WILAYA YA NYASA
0767417597
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa