MANISPAA ya Songea kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kuanzia wiki ya mwisho ya mwezi Machi iliweka kituo cha wananchi kujitolea damu kwenye viwanja vya soko kuu la Songea.
Uchunguzi umebaini kuwa asilimia 80 ya wanaohitaji damu nchini ni wanawake kwa sababu mbalimbali ikiwemo uzazi salama wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida na njia ya upasuaji.
Katika kipindi cha siku tatu za uhamasishaji wa wananchi kujitolea damu,lengo lilikuwa ni kukusanya uniti 100 za damu.Hata hivyo kuanzia Machi 27 hadi 29 kitengo cha damu salama katika kituo cha soko kuu kilikuwa kimekusanya uniti 67.
Changamoto kubwa iliyosababisha kutofikia malengo ya kukusanya uniti 100 kwa siku tatu ni kufungwa kwa shule za sekondari kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu hali ambayo imesababisha watu wazima wachache kujitolea damu salama.
Uchunguzi unaonesha kuwa watu wanaoongoza kujitolea kutoa damu ni wanafunzi wa shule za sekondari na Taasisi kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
Jambo la msingi ni kuendelea kutoa elimu ya kujitolea damu kwa watanzania kwa kutumia vyombo vya habari,matangazo,mikutano ya hadhara hali ambayo inaweza kuhamasisha wananchi wengi kuona umuhimu wa kujitolea damu ili vituo vya afya na hospitali ziwe na benki ya kutosha ya damu salama.
Mpango wa Taifa wa Damu Salama umesema Jamii Kutokuwa na Elimu Juu ya Umuhimu wa Kujitolea Damu, imekuwa ni Kikwazo Namba Moja Kwa Mpango huo Kushindwa Kufikia Malengo ya Ukusanyaji wa Damu Salama Kutoka Kwa Wananchi.
Kuna wanaoamini kwamba kujitolea damu ndio mwanzo wa kubomoa mfumo sahihi wa mzunguko wa damu na kuna wanaoamini kuwa kujitolea damu ndio kujiletea ugonjwa wa shinikizo la damu. Fikra hizo ndizo zinanidhihirishia kuwa katika umma huu wa Watanzania, wapo wasioelewa mambo mengi kuhusu kujitolea damu, hivyo kusababisha utoaji damu kwa hiyari kuwa mgumu.
Kuna umuhimu wa kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha elimu sahihi kuhusu umuhimu wa watu kujitolea damu inawafikia hata wananchi wanaoishi pembezoni.
Maneno yanayozungumzwa na wasioelewa kuhusu umuhimu wa kujitolea damu ni mengi kwa hiyo wahusika waichukulie hiyo kuwa ni changamoto na kuitafutia ufumbuzi ili hatimaye tatizo la upungufu wa damu katika vituo vya kutolea huduma za afya libakie kuwa historia.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari na Mawasiliano Manispaa ya Songea
Aprili pilii,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa