DINI iliyoanza kuingia katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ni dini ya Kikristo,Mwinjilisti wa kwanza wa Anglikana William Parcival Johnson alianza kuhubiri Februari 9,1881 na alihamia rasmi Liuli mwambao mwa ziwa Nyasa mwaka 1906.
Mwinjilisti Johnson alifariki Oktoba 11,1928 na kuzikwa ndani ya Kanisa la Msalaba Liuli ambalo ndiyo kanisa kuu la Dayosisi ya Anglikana Ruvuma.Hata hivyo wakati huo ilitambulika kwa jina la Dayosisi ya Nyasaland,ikafuatiwa na Dayosisi ya Southwest Tanganyika ilipofika Julai saba, 1952 na baadaye iliitwa Dayosisi ya Ruvuma Julai pili,1971.
Kwa mujibu wa Askofu wa Anglikana Dayosisi ya Ruvuma Mhashamu Raphael Haule tangu kuanzishwa kwa Dayosisi hiyo mwaka 1971 kwa mara ya kwanza kanisa hilo mwaka 2017 limebariki na kutamka rasmi kwamba makao makuu ya Dayosisi hiyo yapo Liuli.
Anasema kanisa kuu la Dayosisi ya Ruvuma lilikuwa katika kisiwa cha Likoma nchini Malawi na kanisa kuu shirikishi lilikuwa Liuli Tanzania ambapo Septemba 25,2017,kanisa kuu la Msalaba la Liuli lilibarikiwa kwa ibada maalum ambayo pia ilishirikisha viongozi wa kanisa toka kisiwa cha Likoma nchini Malawi.
Kulingana na Mhashamu Haule Dayosisi ya Ruvuma ina makanisa 135 na mitaa(parokia) 44 na kwamba kanisa lina changamoto kubwa ya mapadre hali ambayo inasababisha padre mmoja kuhudumia makanisa mawili hadi matatu.
“Dayosisi ya Ruvuma imetulia,mitaa yote inafanyakazi za miradi mbalimbali ya kanisa ikiwemo ujenzi wa makanisa na miradi mingine ya maendeleo,tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Dayosisi yetu,tuombeane amani, upendo na umoja ili kuimarisha ushirikiano’’,anasisitiza Mhashamu Haule.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari na Mawasiliano Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa