Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
19.11.2021
Mwenyekiti CCM Wilaya ya Songea Hamisi Abdallah Ally amewataka wakala wa barabara za vijijini na mijini-TARURA kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa kwa lengo la kubaini barabara zinazotakiwa kupewa kipaumbele wakati wa matengenezo.
Hayo yamebainisha wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi-CCM katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kilichofanyika leo tarehe 19 Novemba 2021,Ilani ambayo iliwasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema katika ukumbi wa CCM Wilaya na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama cha mapinduzi pamoja na wataalamu kutoka Manispaa ya Songea.
Hamisi alisema kuwa TARURA inatakiwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa wakati wa matengenezo ya barabara ili kazi ifanyike kwa usahihi na iendane na mahitaji ya wananchi, ambapo alisema, kutoshirikisha viongozi hao kunapelekea kuchonga barabara ambazo hazipo kwenye mtandao na hatimaye kuongeza malalamiko kwa jamii.
Aliongeza kuwa miongoni mwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi ni pamoja na tatizo la miundombinu ya barabara ndani ya Manispaa ya Songea ambapo TARURA wanatakiwa kufanya uboreshaji wa miundombinu hiyo hasa katika maeneo ambayo tayari yalianza kufanyiwa matengenezo. ’Alisisitiza’
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema akiwakilisha taarifa katika kikao hicho, ambapo alinza kwa kusema kuwa “Halmashauri ya Manispaa ya Songea imeendelea kutekeleza Kwa mafanikio Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2020-2025 Kwa kuhakikisha kuwa Serikali katika ngazi zake zote ambazo ni Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaendelea na jitihada za kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo na umasikini, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa, ‘Alibainisha’
Aidha alieleza kuwa katika kutekeleza maelekezo ya Ilani hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Songea inatekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo ni Kilimo na biashara ambapo Kilimo huchangia asilimia 75 ya pato la mwananchi pamoja na kuboresha miundombinu ya kimkakati kama yalivyo maelekezo ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Mgema alisema Serikali ya Wilaya itaendelea kusimamia vyema na kuhakikisha kwamba utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 chini ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan.
Akijibu hoja zilizotolewa na wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Songea Kaimu Meneja TARURA Manispaa ya Songea Davis Mbawala alisema kuwa hadi kufikia Septemba 2021, Halmashauri ya Manispaa ya Songea kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imepokea jumla ya Shs. 509,175,122.59 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara ambapo utekelezaji wa matengenezo ya barabara zote zenye changamoto umeshaanza kulingana na bajeti iliyopo.
Naye Meneja ufundi SOUWASA Manispaa ya Songea alieleza kuwa hadi kufikia Septemba 2021 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi imefikia asilimia 85.3 ya wakazi waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea na bado jitihada zinaendelea ili kuhakikisha maenneo yote yanafikiwa na huduma ya maji safi na salama.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa