MRADI wa Liquefied Natural Gas(LNG) yaani gesi kimiminika unaendelea ambapo Sehemu kubwa ya gesi asilia iliyogunduliwa nchini hadi sasa iko baharini kwenye kina kirefu na inafikia kiasi cha futi za ujazo trilioni zaidi ya 53. Gesi hiyo imegunduliwa takribani umbali wa kilometa 80 mpaka 100 kutoka nchi kavu na kwenye kina cha urefu wa kati ya mita 1,500 na 3,000.
Afisa Mkuu Mwandamizi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini TPDC mhandisi Modesto Lumato anasema jumla ya gesi asilia ambayo imegundulika majini na nchi kavu nchini katika mikoa ya Lindi na Mtwara inafikia futi za ujazo trilioni 57TCF hadi kufikia mwaka 2016 ambapo futi 30 trilioni zinatarajiwa kuuzwa nje ya nchi.
Hata hivyo Mhandisi Lumato anasisitiza kuwa futi za ujazo trilioni moja inaweza kutumika hata miaka 300 hadi 500 na kwamba meli zitaanza kubeba gesi asilia ambayo ni liquidified natural gas mwaka 2021 tayari kwa kuuzwa katika nchi za Japan,China na Ulaya.
Lumato anasema gesi asilia ambayo ni LNG(gesi kimimika) inauzwa nchini Japan ambako kuna soko kubwa la gesi asilia ambapo hapa nchini hivi sasa viwanda 36 jijini Dar es salaam vinatumia umeme wa gesi asilia na magari 70 katika nchi nzima yameunganishwa mfumo wa gesi asilia ambao unapunguza gharama kwa asilima 65 ukilinganisha na mafuta.
Lumato anasema gesi asilia baada ya kuvunwa hahiifadhiwi kama mafuta bali ikishavunwa baharini inatakiwa kuuzwa kwa mteja moja kwa moja.
Kutokana na mazingira hayo na wingi wa gesi hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wawekezaji ipo kwenye mchakato wa kuendeleza gesi asilia hiyo kwa ajili ya matumizi ya ndani na pia kwa ajili ya kuuza nje ya nchi kama Liquefied Natural Gas (LNG).
LNG ni gesi asilia iliyopozwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa hadi kufikia kiwango cha nyuzi joto -161 ambapo huwa rahisi kubeba na kusafirisha. Hata hivyo katika mradi wa LNG,Serikali imeamua mtambo wa uchakataji gesi utajengwa na kuwekwa nchi kavu na sio baharini.
Mradi wa LNG utakapoanza utakuwa na faida nyingi za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa watanzania na kuipatia nchi fedha za kigeni kutokana na mauzo ya gesi nje ya nchi. Faida nyingine za kiuchumi ni pamoja na kuiwezesha Serikali kuendeleza sekta ya umeme na viwanda ikiwa ni pamoja na kufanikisha uanzishwaji wa ukanda wa viwanda (Industrial Park) kwa ajili ya uwekezaji katika viwanda vya kemikali (petrochemicals), saruji, na mbolea.
Lengo kuu la mradi wa LNG ni kuuza na kusafirisha gesi nje ya Tanzania ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia katika bahari ya kina kirefu umesababisha kuanzishwa kwa mradi wa kusafirisha gesi kwa njia ya kimiminika (LNG) kwa ajili ya kuuza kwenye masoko mbalimbali duniani.
Mradi wa gesi asilia utasababisha nchi kupata fedha nyingi za kigeni na kutoa ajira rasmi na ajira ambazo sio rasmi kwa watanzania.Hata hivyo ma,kampuni yanaendelea kuhakiki kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa ili kuwa na uhakika wa kuwepo kwa mradi wa LNG.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo
Mawasiliano albano.midelo@gmail.com,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa