Manispaa ya Songea kukopesha wajasiriamali milioni 48.8
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma mwezi huu inatarajia kukopesha wajasirimali wadogo kiasi cha sh.milioni 48.8.
Mafunzo kwa ajili ya vikundi 66 vitakavyokopeshwa mikopo hiyo yametolewa ili kuhakikisha wajasiriamali hao wanatumia mikopo kwa malengo waliokusudia na kurejesha kwa wakati.
Kati ya vikundi hivyo vinavyokopeshwa,vikundi vya wanawake ni 35 vitakavyokopeshwa sh.milioni 29.6 na vikundi vya vijana 31 ambavyo vitakopeshwa sh.milioni 19.2
Hata hivyo katika kipindi cha mwaka 2016/2017 Manispaa ya Songea inatarajia kukopesha jumla ya sh.milioni 88.8.
Akizungumza katika mafunzo hayo,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Abdul Hassan Mshaweji ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo amesema Manispaa hiyo kila mwaka wa fedha imeendelea kutoa mikopo kwa wanawake na vijana ambapo mwaka wa fedha wa 2015/2016 Manispaa hiyo kupitia mapato ya ndani ilitoa sh.milioni 52.5.
Mshaweji amesisitiza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea itaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dk.John Magufuli ya kuwatetea wanyonge hasa wanawake na vijana ikiwemo kupiga marufuku ushuru ambao unawanyanyasa wananchi wanyonge.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Manispaa hiyo Naftali Saiyoloi amesema mkopo huo unatolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana na kwamba lengo ni kuinua hali ya uchumi katika makundi hayo mawili.
Ameyataja masharti yanayomwezesha mjasiriamali kupata mkopo huo, kuwa ni awe mwanamke au kijana mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na isizidi 35,awe amejiunga kwenye vikundi vya kuanzia watu watano,kikundi kiwe na katiba na mkopo unarejeshwa ndani ya mwaka mmoja kwa riba ya asilimia 10.
Mfuko wa kukopesha wanawake na vijana ulianzishwa mwaka 1993 na kwamba mfuko huo licha ya kuwa na fedha kidogo ,umelenga kuongeza ajira,kuinua uchumi wa mwananchi wa kawaida na hasa vijana na wanawake.
Taarifa imetolewa na
Albano Midelo
Afisa Habari wa Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa