UCHUNGUZI ambao umefanywa katika vijiji vya Mdunduwalo,Lugagara na Litisha wilayani Songea mkoani Ruvuma umebaini kuwa hakuna zahanati yeyote ya serikali ambayo imefungwa kwa kukosa watumishi au zahanati iliyogeuzwa duka.
Diwani wa Kata ya Kilagano ambako kuna zahanati ya Lugagara Emanuel Ngonyani amesema hakuna zahanati ambayo imefungwa katika kijiji cha Lugagara kwa kukosa watumishi badala yake katika kijiji hicho kuna mradi wa zahanati ambao bado haujakamilika.
“Hii zahanati haijafungwa kwa kukosa wahudumu kwa kuwa bado haijafunguliwa,ujenzi wake unaendeleo, tunatarajia baada ya muda sio mrefu zahanati yetu itafunguliwa,hivyo bado haijaanza kutoa huduma”,anasisitiza Diwani Ngonyani.
Naye Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Mdunduwalo kata ya Maposeni Kristina Ntara amesema katika kijiji hicho hakuna zahanati iliyofungwa kwa kukosa watumishi na kwamba wamesikitishwa na taarifa zilizotolewa kuwa katika kijiji hicho kuna zahanati imefungwa kwa kukosa watumishi.
“Nawaomba waandishi wa habari wawe wanachukua taarifa sahihi,nasikitika sana waandishi wameandika zahanati katika kjiji hiki imegeuzwa duka jambo ambalo sio sahihi kwa kuwa ile ni ofisi ya kijiji na wala sio zahanati’’,anasema Ntara.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Dk.Yesaya Mwasubira amesisitiza kuwa miradi yote ya zahanati tatu zilizotangazwa na Kituo cha ITV ipo katika hatua za ujenzi haijakamilika hivyo huwezi kuleta watumishi katika zahanati ambazo hazijakamilika.
Amesema zahanati hizo ujenzi wake ukikamilika ndipo serikali italeta watumishi ambapo amesikitishwa na taarifa za ITV kuwa jengo la zahanati limegeuzwa duka ni habari za uongo na kwamba hakuna msaada aliyotoa mfadhili aliyetajwa katika mradi wa zahanati ya Mdunduwalo.
“Hizi habari za kuwachanganya wananchi kwamba Halmashauri imegeuza zahanati kuwa duka ni habari za uongo,umma ujue hivyo,zahanati zipo katika hatua za kukamilishwa ili kuleta watumishi,tunawaomba ITV wakanushe ni habari za uongo’’,anasisitiza Dk.Mwasubira.
Hata hivyo Dk.Mwasubira amesema kuna zahanati moja ambayo ilikuwa inamilikiwa na misheni katika Kijiji cha Litisha ambayo ilifungwa Novemba mwaka jana kwa kukosa sifa zinazotakiwa na Wizara ya Afya ambapo amesema endapo watatekeleza vigezo na sifa zinazotakiwa na Wizara,zahanati hiyo inaweza kufunguliwa na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.Amesema katika Kijiji hicho kuna mradi wa zahanati ya kijiji ya wananchi ambao bado upo katika hatua za awali za ujenzi.
Mei 20,2018 na Kituo cha Habari cha ITV na mitandao yake ya kijamii iliandika na kutangaza habari ,zilizohusu kufungwa kwa zahanati tatu katika wilaya hiyo kwa kukosa watumishi na zahanati moja kugeuzwa duka.
Akizungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea kuhusiana na taarifa hizo,Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema alisema taarifa hiyo ambayo pia ilisambazwa na kurasa za mitandao ya kijamii ya ITV, imekosa ufafanuzi kuwa mfadhili huyo anazungumzia zahanati zipi ambazo zimefungwa kama zinazomilikiwa na misheni au serikali hali ambayo imesababisha upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii ambayo imeandika kuwa zahanati hizo ni za serikali jambo ambalo sio sahihi.
“Zahanati zetu zote katika vijiji hivyo ambavyo vimetajwa bado ujenzi wake haujakamilika na hazijaanza kutoa huduma,kwa hiyo haiwezekani zahanati au kituo ambacho hakijakamilika kujengwa,kiweze kufungwa kwa sababu ya kukosa watumishi’’,anasisitiza Mgema.
Ameongeza kuwa kituo ambacho kinaweza kufungwa kwa kukosa watumishi ni kile ambacho ujenzi wake ulishakamilika,kimepata usajiri na kimeanza kufanyakazi.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 23,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa