Na;
Amina Pilly;
25 Agosti 2022
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songeaa Dkt. Frederick Sagamiko amewataka wataalamu wa idara ya mifugo na uvuvi kuweka kituo cha kukusanyia maziwa kwa lengo la kufanya kuhakiki ubora wa maziwa ili kuwalinda walaji wa Manispaa ya Songea.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 24 Agosti 2022 katika kikao cha kamati ya lishe ya Halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Songea ambacho kilihudhuriwa na wataalamu wa mbalimbali ikiwa nisehemu ya utekelezaji wa robo ya nne ya mwaka 2022 kwa lengo la kufanya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za lishe.
Dkt.Sagamiko alisema ili kuweza kukabiliana na utapiamlo ni lazima kutekeleza mikakati ambayo itasaidia kuondoa au kupunguza tatizo la utapiamlo kwa kufanya ufuatiliaji wa akina mama wajazito ambao uhudhuria kliniki na kupata elimu ya Lishe ambayo husaidia kuondoa tatizo la kujifungua mtoto mwenye uzito chini ya kilo 2.5.
Amewarai wakuu wa shule zote zilizopo Manispaa ya Songea kuweka bustani za Mboga mboga, pia Wazabuni wote ambao hupeleka chakula shuleni “mafuta ya kupikia, unga, na chumvi” wanatakiwa kuongeza virutubisho lishe kwenye chakula ili kujenga afya za wanafunzi jambo ambalo linawezekana na agizo hili linatakiwa kutekelezeka mara moja. Dkt. Sagamiko alisisitiza.
Alisema Manispaa ya Songea imelenga kutekeleza mpango Mkakati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kuweka kituo cha kulelea watoto wadogo “Day Care” kituo ambacho kitasaidia wananchi ambao kipindi cha masika ya mvua huenda kushiriki shughuli za kilimo cha shambani ambapo watoto wao wataweza kutunzwa kituoni hapo na kupata uangalizi wa kariibu ambapo itasaidia kupunguza tatizo la utapiamlo.
Naye Afisa Lishe Manispaa ya Songea Florentine Kissaka alisema katika kupambana na udumavu na utapiamlo, kitengo kilifanya uchunguzi wa hali ya lishe kwa kutumia mzingo wa mkono kwa watoto walio chini ya miaka mitano pamoja na upimaji wa uzito na umri wa mtoto.
Kissaka alisema hali ya lishe katika robo ya nne ya mwaka 2022 jumla ya watoto 32,492 wenye umri wa chini ya miaka mitano walichunguzwa hali ya lishe kati ya watoto 32,216 sawa na asilimia 100.8% na kati yao watoto 33 waligundulika kuwa na utapiamlo mkali ambao ni sawa na asilimia 0.1%. Aidha watoto 790 ambao ni sawa na 2.4% waliochunguzwa waligundulika kuwa na utapiamlo wa kadiri, pamoja na watoto 31,690waliochunguzwa sawa na 97.5% hawakuwa na utapiamlo. Alibainisha.
Aliongeza kuwa watoto wote waliogundulika na utapiamlo wa kadiri walipewa unasihi wa uandaaji wa chakula na mpangilio wa ulaji unaofaa, pia watoto wote waliokuwa na utapiamlo mkali walipewa rufaa kwenda hospitali ya rufaa Songea kwa matibabu ya utapiamlo (SAM – Management).
Alisema Manispaa ya Songea inaendelea na zoezi la ufuatiliaji na upatikanaji wa mbegu bora za viazi lishe na kufanya utafiti wa maeneo ambayo yanafaa kwa kulimwa mazao ya aina mbalimbali ili kuwa na uzalishaji mkubwa pamoja na kuweka mpango mkakati wa kuongeza vikundi vya ufugaji wa wang’ombe ili mazao ya maziwa yaweze kupatikana kwa wingi zaidi.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa