WATALII toka nje ya nchi wameanza kutembelea hifadhi ya Asili ya Luhira iliyopo katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Takwimu za mwaka 2016/ 2017 zinaonesha kuwa hifadhi hiyo imepokea watalii toka nchi za Ujerumani,Afrika ya Kusini,India,Ufaransa,Italia, Uholanzi na wageni toka mikoa mbalimbali nchini ambao pia wanafanya utalii wa kuchunguza aina ya mimea na ndege katika hifadhi hiyo.
Msimamizi wa Hifadhi hiyo Msonda Simwanza anasema wanajiandaa kuweka mazingira ambayo yatawezesha wanyama kama tembo,simba na wanyama wengine adimu kuishi katika hifadhi hiyo bila kuleta athari kwa wanyama na binadamu.
Simwanza anasema hivi karibuni Hifadhi hiyo imetumia zaidi ya sh. Milioni 15 kuleta wanyama aina ya swalapala watano na pongo wawili toka Hifadhi ya Arusha.
Moja ya vivutio vikubwa vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni hifadhi ndogo ya asili ya wanyama inayoitwa Ruhila Natural Game Reserve yenye ukubwa wa hekta 600 ambayo ilianzishwa mwaka 1973,ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.
Ndani ya Hifadhi hiyo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo pundamilia, fisimaji, nyani,pongo tumbili, kakakuona,swalapala na kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali.
Mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea,simu 0784765917
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa