Anaitwa Kinjekitile"Bokero" Ngwale. Jina maarufu zaidi katika historia ya Tanzania. Ni vigumu kuizungumzia Historia ya vita vya Majimaji pasipo kumtaja Shujaa huyu.
Alizaliwa huko Ngarambe (Umatumbi) Tanzania. Kuhusu tarehe, Mwezi na Mwaka aliozaliwa bado havijawekwa katika kumbukumbu sahihi.
Alinyongwa mwezi Agosti mwaka 1905 na maafisa wa Ujerumani kwa kosa la uchochezi.
Mwanzoni mwa karne ya 20 aliwashawishi watu katika Ukanda wa Kusini ya Tanzania kusimama kidete na kupambana dhidi ya mtutu wa bunduki wa Wajerumani waliokuwa wakiitawala Tanganyika wakati wa ukoloni, akiwaahidi kuwalinda kwa maji ya miujiza.
Mwanaume huyu anachukuliwa kama ishara ya upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ujerumani nchini Tanzania.
Alidai kwamba yeye ni roho na kwa sababu hiyo akawataka watu wa Tanganyika kuwapinga Wakoloni ambapo aliwapa maji aliyodai kuwa na dawa ambayo yangewafanya wasiweze kudhurika.
Inaelezwa kwamba aliipata dawa hiyo kutoka kwa roho aliyejitokeza kwake katika umbile la nyoka, akamburuza Kinjeketile chini ya maji na alipoibuka baada ya saa ishirini na nne, alikuwa amekauka na akaanza kufanya utabiri.
Anafahamika pia kwa kuyaunganisha makabila ya eneo hilo na kadri ujumbe wake ulivyozidi kusambaa, akachangia kuwa mtu wa kwanza kuleta utaifa katika ardhi ya Tanganyika.
Anajulikana pia kwa kuwaambia wafuasi wake kwamba iwapo watatumia maji yake yaliyo na dawa, risasi za Wajerumani hazingewaingia yaani zingeyeyuka.
Anafahamika kwa kuwa mwanzilishi wa vita vya Maji Maji, ingawa yeye mwenyewe alikufa kwa kunyongwa muda mfupi baada ya vuguvugu hilo kuanza.
Kati ya mwaka 1905 na 1907 Vita hivyo vilishika kasi na vilikuwa mojawapo ya vita vikuu dhidi ya ukoloni barani Afrika.
Inakadiriwa kwamba kati ya watu 180,000 hadi 300,000 walifariki dunia wakati wa vita hivyo huku sababu nyinginezo kama njaa na magonjwa zikichagiza zaidi watu kupukutika.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa