Kamati ya Chakula, Dawa na Vipodozi katika Manispaa ya Songea imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi kwa kusisitiza kuzingatiwa kwa muda wa matumizi ya bidhaa hizo.
Kamati hiyo imewataka wananchi kuhakikisha wanazingatia tarehe ya kutengenezwa pamoja na muda wa mwisho wa matumizi ya bidhaa za chakula na vipodozi wanazonunua na kutumia, ili kulinda afya zao na kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zilizopitwa na muda.
Kwa upande wake, TBS Manispaa ya Songea imewataka wafanyabiashara wote kusajili majengo yao kwa hiari kupitia Kitengo cha Afya Kinga, huku ikisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuchukua uzito wa zoezi hilo kwa ajili ya kuboresha usalama wa biashara na afya ya jamii.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo, Mratibu wa kamati ya chakula dawa na vipodozi Salumu Mboga alisema kuwa katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, Kitengo cha Afya Kinga kimefanikiwa kukagua jumla ya majengo 590 yanayojihusisha na biashara ya vyakula na vipodozi, ambapo majengo 101 yamesajiliwa kwa biashara ya vyakula na vipodozi. Zoezi hilo linaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.
Aidha, Idara ya Afya Kinga kupitia Kitengo cha Afya imejipanga kuendelea kufanya ukaguzi wa usafi wa mazingira mara kwa mara, huku ikiwataka wananchi kuzingatia sheria na kanuni za usafi wa mazingira.
Wananchi, hususan wafanyabiashara wa mama na baba lishe, wametakiwa kupima afya kabla ya kuanza biashara, kufyeka nyasi zinazozunguka maeneo ya biashara na makazi yao, pamoja na kudumisha mazingira safi ili kuzuia magonjwa na kulinda afya ya jamii kwa ujumla
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa