Songea, 23 Aprili 2025 Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Mhe. Michael Mbano, imewapongeza wataalamu wa halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Manispaa hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata za Ruhuwiko, Mjimwema, Mjini, na Msamala. Miradi hiyo imeelezwa kuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma kwa wananchi kupitia fedha za mapato ya ndani na wahisani.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni ujenzi wa miundombinu ya stendi ya malori katika eneo la Lilambo, wenye thamani ya shilingi milioni 900 kutoka mapato ya ndani. Aidha, kamati hiyo ilikagua ujenzi wa shule mpya ya Ruhuwiko inayogharimu shilingi milioni 560 kutoka fedha za mradi wa SEQUIP, ambapo mradi huo upo hatua ya ukamilishaji.
Miradi mingine ni pamoja na Umaliziaji wa Kituo cha Afya Subira (milioni 115 – mapato ya ndani), Ujenzi wa duka la dawa katika Kituo cha Afya Mjimwema (fedha kutoka basket funds na user fee), Ukarabati wa stendi ya bajaji (milioni 38 – mapato ya ndani), Ujenzi wa madarasa 5, mabweni 2, na matundu 8 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Emmanuel Nchimbi (milioni 71.4 – fedha kutoka kampuni ya BARRICK).
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Mbano aliwataka wataalamu kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira ya miradi hiyo katika hali ya usafi.
"Tunataka wananchi waone thamani ya kodi zao kupitia miradi hii. Hivyo, usimamizi madhubuti na uwajibikaji ni jambo la msingi," alisisitiza Mhe. Mbano.
Kamati hiyo imeahidi kuendelea kufuatilia na kuhakikisha fedha za umma zinaleta matokeo chanya kwa jamii ya Manispaa ya Songea.
IMEANDALIWA NA;
AMINA PILLY
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa