KAMATI ya Fedha na Uongozi ya Baraza la Madiwani la Manispaa ya Songea, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Gorden Sanga imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika baadhi ya Kata za Manispaa ya Songea.Moja ya miradi hiyo ni mradi wa machinjio ya kisasa unaotekelezwa katika Kata ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kamati hiyo kabla ya kuanza ukaguzi,Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Songea Mhandisi Nicolus Danda amesema mradi wa machinjio ya kisasa unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 3.2.
Amemtaja Mkandarasi wa mradi huo ambaye hadi sasa amelipwa shilingi milioni 600 kuwa ni Kampuni ya Giraffe ambapo mkataba wake ni wa mwaka mmoja ambao umeanzia Julai 2017 na kukamilika Juni 30, 2018.
Mkandarasi wa mradi huo amebainisha mradi huo kuwa umefikia asilimia 50 na kwamba ameomba kuongezewa miezi mitatu ili kukamilisha kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Danda kazi ambazo zinafanyika kwenye mradi huo ni ujenzi wa machinjio yenye urefu wa meta 64 na upana wa meta 24,ujenzi wa zizi lenye uwezo wa kuhifadhia ng’ombe 200 na ujenzi wa uzio,tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita ya 162,000.
Kazi nyingine anazitaja kuwa ujenzi wa nyumba mbili ikiwemo ya daktari wa mifugo na mlinzi,ujenzi wa barabara ya kilometa moja ambayo itazunguka eneo la mradi na ujenzi wa maeneo ya kupaki magari.
Mkandarasi huyo ameomba kuongezewa miezi mitatu ili kukamilisha kazi hiyo na kuzitaja sababu zilizochelewesha mradi huo kuwa ni marekebisho ya michoro na uzio.
Wawakilishi toka Benki ya Dunia mwezi Machi mwaka huu walifanya ukaguzi katika mradi huo na kuridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi huo.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 26,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa