Wajumbe wa Kamati ya siasa wa Mkoa wa Ruvuma wametoa pongezi kwa Mkuu wa shule wa Sekondari ya Wavulana Songea kwa kusimamia ukarabati wa majengo katika kipindi cha mwezi mmoja.
Mkuu wa shule hiyo John Sweke akizungumza na wajumbe wa CCM wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma waliotembelea katika shule hiyo amesema shule ilipokea fedha kutoka ofisi ya TAMISEMI kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 952 kwa ajili ya ukarabati wa majengo na miundombinu
Amesema. taratibu za ukarabati ulianza tarehe 09/05/2019 na kwamba ukarabati wa majengo na miundombinu yake umefanyika kwa kutumia force account na mradi umegharimu kiasi cha Tshs. 872,417,048.00 na umefikia asilimia 98 ya ukamilishaji na wamebakiwa na akiba ya Tshs. 80,000,000 ambazo zinaendelea na ukarabati wa maeneo yasiyofanyiwa ukarabati.
Kulingana na Sweke ,Maeneo yaliyofanyiwa kazi ni ukarabati wa vyumba vya madarasa 24, ukarabati wa mabweni 21, ukarabati wa majengo ya maabara matatu, ukarabati wa kumbi nne, ukarabati wa jengo la utawala, zahanati pamoja na stoo, ukarabati wa nyumba za walimu ambazo ni tatu, ukarabati wa matundu 22 ya vyoo na mabafu 24, ununuzi wa meza 100 na viti 100 vya wanafunzi. Na maeneo ambayo yanaendelea kufanyiwa ukarabati ni kufunga madirisha kwenye vyumba vya madarasa 12 na kazi ya kukamilisha viunga.
Hata hivyo amesema kuwa ukamilikaji wa kazi hiyo umechangiwa na umoja wa walimu wa shule hiyo, mhandisi wa Manispaa aliyeshirikiana nao kila siku pamoja na wananchi ambao wameshiriki katika ujenzi kwa namna tofauti wakiwemo mafundi ambao ni wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake, Mjumbe wa kamati ya Siasa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amesema kuwa wameridhishwa na ukarabati uliofanyika katika shule hiyo ambao ni mfano wa kuigwa katika miradi mingine inayotekelezwa katika Mkoa wa Ruvuma.
“Tunachokiona kinaendana na thamani ya fedha iliyotolewa katika kutekeleza mradi huu.” Amesema Mwisho.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ametoa pongezi kwa Mkuu wa shule na amewaomba viongozi wanaosimamia miradi mbalimbali kuwa waadilifu ili walengwa wanufaike mapema na huduma zinazojengwa.
Shule ya Sekondari ya Wavulana Songea ina idadi ya wanafunzi 820 kidato cha kwanza hadi cha sita. Kati ya hao, wanafunzi 40 ni wenye mahitaji maalum ambao wapo kidato cha kwanza mpaka cha nne. Shule hii ni moja ya shule kongwe Tanzania, iliyoanzishwa mwaka 1950 ikiwa na wanafunzi 30.
Imeandaliwa na
Bacilius Kumburu
Wa kitengo cha TEHAMA Manispaa ya Songea
Agosti 30, 2019
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa