KARAKANA ya useremala ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilianza rasmi mwaka 1986 baada ya kufungwa mitambo ya kulanda mbao kwa ufadhili wa Shirika la NIDA.
Kulingana na taarifa ya karakana hiyo mwaka 1992 ilipata ufadhili mwingine wa mitambo na wataalam toka Shirika la Maendeleo la Ujerumani(GDS) kwa kuongeza mitambo na vifaa vya mikono hali iliyosababisha karakana hiyo kujiendeshakibiashara.
Karakana ya Manispaa ya Songea bado inatoa mchango wa pato la Halmashauri na kufanya kazi nyingine za huduma kwa Halmashauri ikiwemo utengenezaji wa madawati na meza kwa ajili ya shule za msingi na sekondari.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018,karakana ya Manispaa ya Songea ilipangiwa kukusanya shilingi milioni sita ambapo hadi sasa imefanikiwa kukusanya shilingi milioni 4.88 sawa na asilimia 81.
Licha ya mafanikio hayo,karakana hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutolipwa kwa baadhi ya madeni ambapo hadi sasa zinadaiwa zaidi ya shilingi milioni 3.4 toka kitengo cha biashara,Idara ya Utawala,Idara ya Elimu Sekondari na Idara ya Afya.
Karakana ya Manispaa ya Songea iwapo itapewa ruzuku ya kutosha itaweza kununua malighafi na vitendeakazi vya kutosha sanjari na kuwalipa vibarua hali ambayo inaweza kuongeza uzalishaji hivyo kuchangia zaidi mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Juni 28,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa