Kituo cha afya Mjimwema kuwa hospitali ya Manispaa ya Songea KITUO cha Afya Mjimwema kilichopo katika Manispaa ya Songea,kinatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji wakati wowote hivyo kuwa na hadhi ya hospitali. Daktari Mkuu wa Manispaa ya Songea Dk.Simon Chacha amesema jengo la upasuaji limekamilika na baadhi ya vifaa vimefika ambapo hivi sasa zinahitajika zaidi ya sh.milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha kifaa cha upasuaji ili huduma hiyo ianze mara moja . Amesema huduma ya upasuaji ikianza itawezesha Kituo hicho kuwa na hadhi ya Hospitali ambayo maombi ya kuwa hospitali tayari yapo Wizara ya Afya.Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepitisha ombi la kituo cha afya cha mji mwema kupandisha hadhi kuwa hospitali ya Halmashauri ya manispaa hiyo. Ombi hilo liliwasilishwa katika Baraza la madiwani ili Halmashauri iridhie hatua nyingine ziendelee hatimaye Halmashauri ya Manispaa hiyo iwe na Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo ombi la kupandisha hadhi Kituo hicho cha afya lilikuwa ni agizo la Waziri wa Afya,Ustawi wa Jamii,jinsia,Watoto na Wazee Ummy Mwalimu alipotembelea kituo hicho Januari 11 mwaka 2016. Waziri Mwalimu aliagiza Ombi la kupandisha hadhi Kituo cha Afya Mjimwema kuwa Hospitali ya Wilaya liwasilishwe Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee ili kupata idhini ya Wizara yenye dhamana. Kikao cha Baraza la madiwani kikiongozwa na Mstahiki Meya Abdul Hassan Mshaweji kilipokea taarifa na kikao kiliidhinisha u pandishaji hadhi Kituo cha Afya Mjimwema kuwa Hospitali ya Halmashauri ya manispaa.
Taarifa imetolewa naAlbano Midelo
Afisa Habari na Mawasiliano Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa