IKIWA ni takribani wiki moja imepita hadi sasa tangu umeme wa Grid ya Taifa ulipowashwa katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amezidua kiwanda kipya kilichojengwa katika kata ya Ruhuwiko Manispaa ya Songea chenye uwezo wa kusaga mahindi tani 30 ambayo ni sawa na magunia 300 kwa siku.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Alhaj Abdul Hassan Mshaweji akizungumza katika mkutano wa Baraza maalum la madiwani wa Manispaa hiyo wenye lengo la kuwasilisha taarifa za Hesabu za kufunga mwaka 2017/2018,amesema kiwanda hicho kimezinduliwa wakati muafaka kwa sababu hivi sasa kitapunguza changamoto za soko la mahindi katika manispaa ya Songea na mkoa wa Ruvuma na kutoa ajira kwa vijana.
Amesema licha ya kiwanda hicho hivi karibuni mwekezaji mwingine Mohamed Enterprises anatarajia kufungua kiwanda cha kusaga mahindi chenye uwezo wa kusaga mahindi tani 100 kwa siku hali ambayo itazalisha ajira mbalimbali kwa vijana na kupunguza tatizo la soko la mahindi ambalo ni changamoto kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma ambao wanazalisha mahindi kwa wingi.
Sera ya uchumi wa viwanda katika Manispaa ya Songea ambayo imeanzishwa na Rais wa Awamu ya tano sasa inatekelezwa kwa vitendo katia manispaa ya Songea ambapo hadi sasa manispaa hiyo ina jumla ya viwanda 500 vilivyogawanyika katika makundi manne ambayo ni viwanda vikubwa sana,viwanda vya kati,viwanda vidogo na viwanda vidogo sana.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Septemba 22,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa