MOJA ya vivutio vikubwa vya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni hifadhi ndogo ya asili ya wanyama inayoitwa Ruhila Natural Game Reserve yenye ukubwa wa hekta 600 ambayo ilianzishwa mwaka 1973,ipo umbali wa kilometa saba kutoka mjini Songea.
Ndani ya Hifadhi hiyo kuna aina mbalimbali za wanyama wakiwemo pundamilia, fisimaji, nyani,pongo tumbili, kakakuona,swalapala na kobe,pia bustani hiyo ni makazi ya reptilia na ndege wa aina mbalimbali.
Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kikosi dhidi ya Ujangili Kanda ya Kusini Msonda Simwanza anasema ndani ya Hifadhi ya Luhira kuna aina mbalimbali za mimea ya asili ikiwemo miombo, minyonyo, mininga, mikusu, migunga, miwanga, mizambarau, mirama, mitunduru,misasa,miviru na mikuyu.
“Ndani ya Luhira,mtalii anaweza kufanya utalii wa kutembea kwa miguu,kupiga picha,kuangalia wanyama na ndege,utalii wa kuweka kambi(camping) na kufanya mapumziko ya mchana(picnic) hufanyika ndani ya eneo maalum’’,anasema.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa wakati hifadhi hiyo inaanzishwa ilikuwa mbali na makazi ya binadamu ambapo hivi sasa ipo umbali wa kilometa sifuri na makazi ya watu.
Msimamizi Mkuu wa Hifadhi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Kusini wa Kikosi dhidi ya Ujangili Simwanza anasema kutokana na uharibifu,huo wa mazingira uliosababishwa na shughuli za kibinadamu wakazi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo wamekuwa wakitegemea uoto wa asili uliohifadhiwa katika hifadhi hivyo kuhatarisha uwepo wake.
Kulingana na Simwanza,hifadhi hiyo wakati inaanzishwa kulikuwa na wanyama na ndege mbalimbali ukiachilia mbali mimea na mito kama vile kapala, nakuchundu, nakala na mto Ruhila ambao ndiyo chanzo cha hifadhi hiyo kuitwa jina la Ruhila
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Aprili 12,2018.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa