NA,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
12.10.2021
Mkoa wa Ruvuma utaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mbolea duniani ambayo hufanyika kila mwaka ifikapo tarehe 13 Oktoba.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya mbolea duniani Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya uthibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) Dkt.Stephen Ngailo alisema kuwa kwa mwaka huu maadhimisho hayo yameanza mapema hapo jana tarehe 11 Oktoba 2021 kuelekea siku ya kilele ambayo tarehe 13 Oktoba 2021 kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau wa mbolea hususani wakulima na wafanyabiashara wa mbolea kwa mapana zaidi ili waweze kujua mifumo mbalimbali ya upatikanaji, usambazaji na matumizi sahihi ya mbolea.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi nchini Tanzania kwa asilimia 75%, hali ambayo imesababisha maadhimisho ya siku ya mbolea duniani mwaka huu kufanyika kitaifa Mkoani Ruvuma ili kutoa hamasa zaidi kwa wakulima kuendelea kuwekeza katika sekta ya Kilimo.’Ngailo Alibainisha’
Naye Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Balozi Wilbert Ibuge alisema kwamba Serikali inaendelea kuboresha sekta ya kilimo nchini ili kuleta mapinduzi halisi kwa maendeleo ya wananchi na kuhakikisha pembejeo bora za kilimo ikiwemo mbolea zinapatikana kwa wingi na kwa wakati.
Ibuge alibainisha kuwa kwa mwaka 2020/2021 Mkoa wa Ruvuma umezalisha tani milioni 1.6 ya mazao ya chakula na biashara sawa na asilimia 91% ya makadirio ya awali ambayo yalikuwa ni kupata zaidi ya tani milioni 1.7, ambapo mazao ya biashara ambayo ni ufuta, soya na mbaazi yamefanikiwa kuingiza mapato kwa kiasi cha shilingi bilioni 16 ambayo yalinunuliwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Alisema kwamba Mkoa wa Ruvuma umeweka mkakati wa utekelezaji wa sera ya kilimo cha biashara kwa mazao ya Soya na Alizeti kupitia mpango wa kilimo cha pamoja (block farming), ambapo alitoa wito kwa wadau mbalimbali na wakulima wote kujitokeza kushiriki na kuwekeza katika kilimo hicho.”Alisisitiza”
Ibuge alihitimisha kwa kuwahamasisha wananchi wote Mkoani Ruvuma kushiriki kikamilifiu katika zoezi la sense ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika Agosti 2022 ili kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahii za idadi ya watu na kuweza kupanga mipango madhubuti kwaajili ya maendeleo.
Pia ametoa rai kwa wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kutumia vitakasa mikono na barakoa pamoja na kuhakikisha wanapata chanjo kwa hiyari ambayo inatolewa bure katika vituo vyote vya afya.
Maadhimisho ya siku ya mbolea duniani Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Mkoani Ruvuma ifikapo tarehe 13 Oktoba 2021 katika uwanja wa Majimaji na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ambapo kauli mbiu ni;
“TUMIA MBOLEA BORA KWA TIJA NA KILIMO ENDELEVU”
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa