Na,
AMINA PILLY,
AFISA HABARI MANISPAA.
15 JUNI 2022
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Ibuge ametoa pikipiki 286 kwa Maafisa kilimo pamoja na Maafisa ushirika Mkoani Ruvuma.
Ibuge ametoa pikipiki hizo hapo jana tarehe 14 Juni 2022 katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa kilimo Mkoani Ruvuma.
Akizungumza wakati akikabidhi pikipiki hizo, Ibuge aliseema kuwa “Pikipiki hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia malengo ya Serikali katika utekelezaji wa sera ya kilimo chenye tija nchini Tanzania kwa manufaa ya wakulima pamoja na kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla”
Aliongeza kuwa pikipiki hizo zimetolewa ili kuwawezesha maafisa kilimo na ushirika kuwafikia wakulima kwa urahisi kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao kwa kutoa ushauri kulingana na aina ya udongo, mbegu inayotakiwa pamoja na aina ya mbolea kwa zao husika.
Amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote 8 Mkoani Ruvuma kuhakikisha wanasimamia utunzaji wa pikipiki hizo ikiwemo na utoaji wa mafuta pamoja na kupeleka pikipiki hizo matengenezo ya kawaida kila wakati.
Ibuge amewataka Maafisa ushirika kuhakikisha wanaimarisha vyama vya msingi vya ushirika kwa kuvitembelea na kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili pamoja na kuzitatua ili kuongeza tija hasa katika kilimo biashara.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema amewataka maafisa kilimo kutumia pikipiki hizo ili kuwafikia wakulima hasa katika maeneo ya pembezoni mwa mji kwa lengo la lutoa elimu ya kilimo na kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao mengi kwa kufuata ushauri wa wataalamu hao.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kutoa pikipiki hizo ambazo zitasaidia kuimarisha sekta ya kilimo Ruvuma ambapo amewataka Maafisa kilimo hao kuhakikisha usalama na utunzaji wa pikipiki hizo.’Alisisitiza’
Kwa upande wake Afisa kilimo Manispaa ya Songea Zawadi Nguaro alisema kuwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepokea pikipiki 28 kwa ajili ya Maafisa kilimo, umwagiliaji na ushirika 28.
Nao Maafisa kilimo Mkoani Ruvuma wametoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutatua changamoto ya usafiri iliyokuwa inawakabili ambapo pikipiki hizo zitawarahisishia kufika maeneo yote ya wakulima na kuongeza tija katika sekta ya kilimo Mkoani Ruvuma.
Mwisho.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa