BATA aina ya tandawala machaka(Denihams bustard) wenye uwezo wa kuruka toka Bara moja hadi jingine inaaminika wanapumzika kwa mwezi mmoja katika bwawa lillilopo Kihagara Mwambao mwa ziwa Nyasa Mkoa wa Ruvuma.
Mhifadhi toka Hifadhi ya Taifa ya Kitulo Godfrey Kyando anasema katika tamasha la fursa za utalii mwambao mwa ziwa Nyasa,imebainika kuwa wakazi wa Kijiji hicho kila mwaka mwezi Septemba wanawaona bata hao ambao wanakuwepo kwa muda kisha wanaondoka.Wakazi wa Kijiji cha Kihagara walionesha eneo ambalo bata hao wanapumzika kabla ya kuendelea na safari.
Hata hivyo Mhifadhi Kyando anasema ndege hao wanafika kwa ajili ya kutaga na kuangua vifaranga katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo iliyopo wilayani Makete Mkoa wa Njombe kuanzia Machi hadi Julai kila mwaka kisha wanaruka na kwenda katika maeneo mengine duniani.
Hifadhi ya Taifa Kitulo inayopita katika mikoa ya Mbeya na Njombe ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 2005 ikijumuisha sehemu ya eneo la shamba la mifugo,msitu wa Livingstone na bonde la Numbi.
Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 442 ndani ya mwinuko wa kati ya mita 2100 hadi 3000,awali ilijulikana kama Elton Plateau baada ya Mvumbuzi Fredirick Elton kupita eneo hili mnamo mwaka 1870.
Mwaka 1960 Shirika la Chakula na Kilimo(FAO) lilichukua eneo hili kwa ajili ya ukulima wa ngano na ufugaji wa kondoo.
Kyando anabainisha kuwa kutokana na umuhimu wa eneo hili wadau mbalimbali wa mazingira walipendekeza eneo hili litangazwe kuwa hifadhi ya Taifa ili kulinda umaridadi wa maua,ndege na mimea adimu inayopatikana ndani ya eneo hili.
Utafiti unaonesha kuwa kuna bata aina ya tandawili machaka ambao waliwekwa alama walipokuwa katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo,walionekana na alama zao katika hifadhi moja barani Australia.Mhifadhi Kyando anasema,utafiti huu ndiyo uliothibitisha kuwa ndege aina hiyo wanasafiri umbali mrefu kwa kuruka toka bara moja kwenda bara jingine.
Utafiti pia umebaini kuwa Katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo kuna ndege aina ya abdims stock,denhams(tandawili machaka) na blue swallow ambao wametoka Afrika ya kaskazini,Afrika ya kusini, Australia na Ulaya ambao wanaitumia hifadhi ya Taifa ya Kitulo kama makazi yao katika misimu tofauti.
Anabainisha zaidi kuwa watalii wakiwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kitulo wanaweza kuangalia ndege hao katika ziwa Zambwe,kuweka kambi kwa ajili ya malengo mbalimbali, utalii wa kutembea kwa miguu,kupanda farasi, michezo ya gofu na kukwea milima.
Makala imeandikwa na Albano Midelo
mawasiliano albano.midelo@gmail.com,simu 0784765918
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa