Maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma yamepamba moto kwa kuhakikisha miradi yote inayotarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa inakamilika mapema.
Wakuu wa Idara,vitengo,maafisa watendaji wa Mitaa na Kata katika Manispaa ya Songea Aprili 30 mwaka huu wamekutana kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea kujadiliana kuhusu miradi 11 iliyopendekezwa kingie kwenye ratiba ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu.
Mwenge wa Uhuru katika Manispaa hiyo unatarajiwa kuingia Juni 7,2018,ukitokea Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambao utapokelewa katika shule ya msingi Mang’ua Kata ya Lilambo na kukimbizwa katika maeneo mbalimbali yenye miradi kisha kukesha katika Soko la Mjimwema kata ya Mjimwema na hatimaye kukabidhiwa Halmashauri ya Madaba Juni 8 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mwenge wa Uhuru Manispaa ya Songea Yonas Faraja,Manispaa ya Songea imependekeza miradi 11 ambayo inatarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa.
Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Songea ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa wilaya hiyo Pololet Mgema na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Tina Sekambo inaendelea kukagua miradi yote ambayo inatarajiwa kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa katika manispaa hiyo.
Mwenge wa Uhuru umelenga kuleta hamasa ya kuleta mabadiliko kwa kuhamasisha miradi mbalimbali ya maendeleo ili wakazi wa Songea na watanzania kwa ujumla waweze kupata maendeleo endelevu.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei Mosi,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa