NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Josephat Sinkamba Kandege yupo mkoani Ruvuma ambapo anatembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI amekagua mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa katika Kata ya Tanga manispaa ya Songea.
Mradi huo ambao umefikia Zaidi ya asilimia 60 unatarajia kukamilika Oktoba mwaka huu ambapo hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa Zaidi milioni 900 ambayo ni asilimia 35 ya malipo ya mradi huo ambao unagharimu Zaidi ya bilioni 3.2.
Akitoa taarifa ya mradi huo,Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Manispaa ya Songea Mhandisi Nicolus Danda amesema mradi wa machinjio ya kisasa unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi bilioni 3.2.
Amemtaja Mkandarasi wa mradi huo ambaye hadi sasa amelipwa shilingi milioni 900 kuwa ni Kampuni ya Giraffe ambapo mkataba wake ni wa mwaka mmoja ambao umeanzia Julai Mosi 2017 na kukamilika Julai mosi, 2018.
Hata hivyo Mkandarasi huyo ameomba kuongezewa miezi mitatu ili kukamilisha kazi hiyo na kuzitaja sababu zilizochelewesha mradi huo kuwa ni marekebisho ya michoro,kuchelewa kukabidhiwa mradi na kuongezeka kazi za ziada ikiwemo uzio na barabara.
Kwa mujibu wa Danda kazi ambazo zinafanyika kwenye mradi huo ni ujenzi wa machinjio yenye urefu wa meta 64 na upana wa meta 24,ujenzi wa zizi lenye uwezo wa kuhifadhia ng’ombe 200 na ujenzi wa uzio,tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita ya 162,000.
Kazi nyingine anazitaja kuwa ujenzi wa nyumba mbili ikiwemo ya daktari wa mifugo na mlinzi,ujenzi wa barabara ya kilometa moja ambayo itazunguka eneo la mradi na ujenzi wa maeneo ya kupaki magari.
Wawakilishi toka Benki ya Dunia mwezi Machi mwaka huu walifanya ukaguzi katika mradi huo na kuridhishwa na viwango vya ujenzi wa mradi huo.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa