MADINI yenye thamani kubwa aina ya shaba ya bluu(blue copper)yamegundulika katika kata ya Mbesa tarafa ya Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.Kugundulika kwa madini hayo kunaifanya wilaya ya Tunduru kuwa ndiyo wilaya pekee nchini na Afrika mashariki na kati kuwa na madini ya shaba ya bluu.
Utafiti umebaini kuwepo kwa madini ya shaba ya bluu karibu tarafa nzima ya Nalasi hadi mto Ruvuma mpakani na nchi jirani ya Msumbiji na pia madini hayo yamesambaa hadi mpakani na wilaya ya Namtumbo.
Wataalamu wa madini wanaelekeza kuwa madini ya shaba ya bluu yana thamani kuzidi madini ya shaba aina nyingine zote ikiwemo shaba nyekundu ambayo inachimbwa katika nchi jirani ya Zambia.
Hivi sasa wachimbaji wadogo wadogo wa madini hayo wapo katika eneo hilo la madini tangu mwaka 2010 na kwamba utafiti kuhusiana na madini hayo bado unaendelea kabla ya serikali kupitia wizara ya nishati na madini kuanzishwa rasmi mgodi wa madini hayo.
Utafiti wa awali wa kijiolojia uliofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1988 katika eneo la Kata ya Mbesa wilayani Tunduru, ulibaini kuwepo kwa madini mengi aina ya shaba ya bluu(Blue copper).Utafiti huo ulifanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ambao ulionesha kuwepo kwa madini aina ya shaba ya bluu ambapo utafiti wa karibuni umebaini kuwepo ubora wa mashapo ya shaba ya bluu katika eneo hilo.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo ina utajiri mkubwa wa madini mbalimbali ambayo yakichimbwa kwa vifaa vya kisasa yanaweza kuufanya mkoa kupanda juu kiuchumi na wananchi wake wakaondokana na umasikini.Miongoni mwa Madini yanayopatikana katika mkoa wa Ruvuma ni makaa ya mawe yaliopo katika wilaya za Mbinga na Songea,madini ya vito yaliyopo wilaya za Tunduru,Mbinga,Namtumbo na Songea na madini ya dhahabu ambayo yanapatikana Mpepo na Ruhekei wilayani Mbinga na madini ya uranium ambayo yanapatikana kwa wingi wilayani Namtumbo.
Mwandishi wa makala haya ni Albano Midelo
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa