BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma limeunga mkono kusitisha nia ya kuanzisha Bodi ya Mfuko wa Elimu katika Manispaa hiyo.
Wakizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songeachini ya Mwenyekiti Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Alhaj Abdul Hassan Mshaweji,wajumbe wameunga mkono uamuzi huo.
Mapendekezo ya kutunga sheria ya uanzishaji wa Bodi ya Mfuko wa Elimu katika Manispaa ya Songea yalifutwa tangu Julai 16 mwaka huu kutokana na mapendekezo hayo kutokubalika na wananchi ikiwemo ada ya shilingi 10,00 kwa mwaka kuchangiwa na kila mwananchi.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea,Mwenyekiti wa kikao hicho Alhaji Mshaweji amewaomba radhi wananchi wa manispaa ya Songea kwa usumbufu walioupata katika rasimu hiyo na kwamba lengo lilikuwa kupata maoni kwa wananchi katika mitaa na kata.
“Tunawaomba radhi wananchi wa Manispaa,lengo lilikuwa ni kutafutia usumbufu tatizo la elimu,wenzetu wilaya ya Tunduru wanachangia mfumo wa elimu kwa kukatwa kila mwaka katika zao la korosho,kwa hiyo tumesitisha kwa sasa mapendekezo hayo’’,amesisitiza Mshaweji.
Kwa upande wake Mbunge wa Songea mjini Dk.Damas Ndumbaro akizungumzia sakata hilo,amesema lengo la rasmu hiyo lilikuwa ni kuboresha lakini kwa upande wa pili lilikuwa linagusa mfuko wa wananchi na kwamba limeleta dosari katika manispaa ya Songea.
“Kosa lililofanyika hapa ni ushirikishwaji kwa sababu Manispaa hii inaundwa na watendaji na wanasiasa, watendaji wanalifahamu vizuri jambo hili lakini wanasiasa hawalijui, maswali wanaulizwa wanasiasa, ushauri wangu jambo likipita kwenye Kamati ya Fedha na Uongozi kabla halijatoka nje lipite kwanza kwenye Baraza’’,anasisitiza Dk.Ndumbaro.
Kwa upande wake Diwani Chikwale anasisitiza kuwa rasimu hiyo imeleta usumbufu mkubwa kwa wananchi katika kata na mitaa na kwamba wanawaona kwamba madiwani wameshindwa kuwatetea wananchi.
Hata hivyo Mstahiki Meya amesisitiza kuwa kulikuwa na upotoshaji mkubwa katika rasimu hiyo ambapo hivi sasa unaandaliwa mpango wa kuhakikisha kuwa madiwani wote wanaelewa vizuri suala hilo kabla ya kwenda kwenye mitaa na kata.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Julai 19,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa