Mambo yafuatayo yanatakiwa kuzingatia wakati wa kununua ardhi au eneo lisilopimwa ili kuepusha usibomolewe nyumba yako.Unaweza kununua na kujenga kiwanja ambacho hakijapimwa katika maeneo ya mjini ili usipate athari zingatia yafuatayo.
KWANZA wasiliana na Ofisi ya Ardhi ya Halmashauri husika ili kuulizia mahali ambapo unataka kununua kiwanja hicho hawajapanga matumizi mengine tofauti ya makazi,kwa sababu unaweza kununua kiwanja kwenye eneo ambalo limepangiwa matumizi mengine kama vile viwanda au dampo,ukalazimika kuhamishwa na kupata hasara.Usifanye haraka kununua kiwanja kisa unauziwa kwa bei nafuu ,jiridhishe kwanza ndipo ununue.
PILI Wasiliana na Uongozi wa Mtaa hasa Mwenyekiti wa Mtendaji wa Mtaa.Watu wengi wanafanya makosa ya kutowashirikisha viongozi wa Mtaa wakati wa kununua kiwanja.Mara kadhaa mtu anafika na fedha zake anamlipa mwenye kiwanja kisha anaondoka.Kununua kiwanja bila kuwashirikisha viongozi wa mtaa unaweza kuuziwa kiwanja kilichouzwa kwa mtu mwingine na kujikuta kiwanja kimoja kinamilikiwa na watu wawili au watatu.
Viongozi wa Mtaa ni muhimu kuwashirikisha kwa kuwa wanaalikwa kwenye mauziano ya viwanja vya watu wao wa mtaa kwa hiyo viwanja vingi wanavifahamu.Ili kujiridhisha iwapo utawapata majirani wa kiwanja unachotaka kununua litakuwa jambo jema zaidi kwa kuwa watakuhakikishia mipaka ya kiwanja hicho.Kumbuka kuandika Mkataba wa mauziano na mashahidi wawepo na watie sahihi kwenye Mkataba huo ili mambo yakigeuka baadaye usiathirike.
Ukiwa na viongozi wa Mtaa,hakikisha kiwanja chako kina barabara inayofika kwenye kiwanja hicho au hakikisha kiwanja hicho hakipo karibu sana na barabara kwa kuwa baadaye kinaweza kukatwa ili kupisha barabara.Waulize viongozi wa Mtaa wamependekeza barabara ipite sehemu gani na itakuwa na upana gani katika barabara ya Mtaa hakikisha isipungue mita kumi ili ramani ya mipango itakapochorwa isikuathiri sana.
TATU unapomaliza kununua uanze mara moja kukiendeleza kiwanja chako kwa kupanda miti,weka fensi au nguzo kwenye kila kona ya kiwanja ili watu wengine wasijekukuingilia.Hakikisha kiwanja chako unakiendeleza mapema kwa sababu ukichelewa unaweza kukuta mgogoro.Usikiache kiwanja kitupu kwa muda mrefu kwa kuwa jirani yako anaweza kukimega au mtu mwingine kukivamia kujenga.
Zingatia vipimo wakati wa kujenga nyumba hasa kiwanja chako kama kipo pembeni ya barabara,nyumba isiwe karibu na barabara,isogeze nyuma ya kiwanja.Unatakiwa uache meta moja na nusu toka kila upande wa mipaka ya kiwanja chako ili kuacha mpenyo kati ya kiwanja na kiwanja,pia unashauriwa kuacha angalau meta tatu hadi tano toka barabarani kutegemeana na ukubwa wa kiwanja chako.
TAFADHARI FUATA SHERIA KWA MAKAZI BORA.
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa