IDARA ya maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji chini ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji awamu ya kwanza (WSDP I)
Mwandisi wa Maji katika Halmashauri Mhandisi Samwel Sanya anasema Halmashauri hiyo imetekeleza miradi ya maji katika mitaa tisa ambayo ni Mahilo, Chandarua, Muhombezi, Mahinya, Ngandula, Muungano, Ruhuwiko kanisani, Mitendewawa na Luhirakati.
“Hadi sasa ujenzi wa miradi ya maji ya Mahilo, Chandarua, Muhombezi, Mahinya, Ngandula, Muungano, Ruhuwiko Kanisani imekamilika kwa asilimia 100 ambayo imegharimu jumla ya 1,656,786,632/ na wananchi wa mitaa hivi wanaendelea kupata huduma ya maji safi ya bomba’’,anasisitiza Mhandisi Sanya.
Hata hivyo amesema miradi ya maji katika mitaa ya Mitendewawa na Luhilakati imekamilika kwa asilimia 80 na kwamba wakandarasi wameendelea kupewa maelekezo ya kukamilisha kazi chache zilizobakia, za ununuzi wa pampu zinazotumia nguvu ya mionzi ya jua na kuzifunga ili miradi iweze kutoa huduma kwa wananchi wa mitaa hiyo.
Kwa mujibu wa Mhandisi huyo,Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Manispaa ya Songea katika bajeti yake imepanga kujenga miradi katika mitaa 15 ambayo ni Nangwahi, SubiraKati, Kihekwa, Kisiwani C, Lami, Mwengemshindo, Pambazuko, Mletele, Mdundiko, Makemba, Nonganonga, Liwumbu , Mjimwema, Makomboni na Mawanja ambapo miradi katika mitaa hiyo ipo katika hatua tofauti tofauti ya utekelezaji.
Amesema miradi ya Mwengemshindo- Pambazuko,imefika Zaidi ya asilimia 30 ya utekelezaji, miradi ya Nangwahi, Subirakati, Kihekwa, Kisiwani C, na Lami imefika Zaidi ya asilimia 25 ya utekelezaji na miiradi ya Mletele, Mdundiko, Makemba, Nonganonga, Liwumbu , Mjimwema, Makomboni na Mawanja imefika asilimia tano ya utekelezaji.
“Katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimepokelewa jumla ya sh. 89,008,080.00 ambapo sh. 48,008,080.00 zilikuwa kwa ajili ya kumlipa mkandarasi wa mradi wa maji ya Ruhuwiko Kanisani na kwa ajili ya usimamizi, usanifu wa miradi na ufuatiliaji sh.26,000,000.00 kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji na Sh.15,000,000.00 kwa ajili ya kampeni ya usafi wa mazingira’’,anasema.
Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji pembezoni mwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ni asilimia 46.6 ambapo watu wapatao 42,279 ndio wanaopata huduma ya maji safi na salama kati ya watu 90,730. Jumla ya vituo vya kuchotea maji ni 249 na vituo vya kuchotea maji vinavyofanya kazi ni 190.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 22,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa