Na;
AMINA PILLY;
AFISA HABARI MANISPAA YA SONGEA.
18 Januari 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema, amewataka maafisa kilimo wote Manispaa ya Songea kuacha tabia ya kukaa ofisini hususani katika msimu huu wa kilimo badala yake wanatakiwa kuwatembelea wakulima kwenye mashamba yao ili kutoa elimu sahihi ya kanuni za kilimo.
Hayo yametamkwa leo 18 januari 2022 wakati wakukabidhi Pikipiki 3 kwa Maafisa kilimo 3 watatu kwa lengo la kutoa huduma bora na kuwafikia wakulima wote kwa wakati husika pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na yenye kuleta tija kwa jamii..
Pololet alisema Halmashauri ya Manispaa ya Songea yenye kata 21 ambapo kati ya kata hizo ni kata 11 tu za kilimo ambazo huzalisha mazao ya nafaka kama mahindi, kahawa,maharage, na kilimo cha mbogamboga.
Aliongeza kuwa ili kufanikisha kuwafikia wakulima wote kwa wakati Manispaa ya Songea imetenga bajeti ya fedha kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kununua pikipiki 6 za magurudumu mawili kwa maafisa kilimo kata 6, fedha zitokanazo na mapato ya ndani ambaPo mpango huo umeanza kutekelezwa leo kwa kuwakabidhi pikipiki 3 maafisa kilimo kata 3.
Pololet alisema ” Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge alizindua Mkakati wa kilimo cha pamoja Mkoani Ruvuma ambacho kinahitaji kusimamiwa kwa ukaribu na wataalamu wa kilimo, hivyo maafisa kilimo mliopewa vitendea kazi mnapaswa kuonesha utendaji kazi wenye tija ili kutofautisha wale wataalamu wasiokuwa na kitendea kazi (usafiri).” Alisisitiza.
Ametoa rai kwa maafisa kilimo hao kutumia pikipiki hizo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kiofisi ya kila siku na kutotumia usafiri huo kama biashara maarufu bodaboda au matumizi binafsi.
Amempongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea Michael Mbano na wataalamu wote wa Manispaa ya Songea kwa kuandaa mpango na bajeti ya kununua usafiri wa pikipiki kwa maafisa kilimo kata 6.
Naye Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano alisema Manispaa ya Songea imetenga bajeti ya shilingi milioni 18, 000,000 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kununua pikipiki 6 ili kuboresha utendaji wa kazi za maafisa kilimo ambapo kwa awamu ya kwanza zimegawiwa pikipiki 3 bado 3 ambapo utekelezaji wake utakamilishwa ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Maafisa kilimo hao wametoa shukrani kwa serikali kwa kuwawezesha vitendea kazi ambapo wameahaidi kutumia vizuri vitendea kazi hivyo na kuboresha utendaji wao wa kazi za kila siku.
Mwisho
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa