HALI ya upatikanaji wa chakula katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma inaridhisha ambapo kuna jumla ya Hekta 24,340.8 ambazo zililimwa msimu wa 2016/2017 na kuzalisha tani 98,671.76. wakati mahitaji ya chakula ni tani 58,280 hivyo kufanya kuwa na ziada ya tani 40,391.76 sawa na asilimia 69.3
Mkuu wa Idara ya Kilimo na Umwagiliaji katika Manispaa ya Songea Zawadi Nguaro anasema Manispaa ya songea inazalisha zao la Kahawa kama zao kuu la biashara na kwamba kuna mpango wa kuotesha miche ya kahawa 143,384 katika vitalu 6 kwa msimu wa 2018/2019.
Amesema Miche 121,784 inatarajiwa kupandwa katika ukubwa Hekta 72.94 na wakulima 290 watanufaika. Hali hii itasaidia kuboresha na kuinua kipato cha wananchi katika kaya zao.
Nguaro anayataja mazao mengine ya biashara yaliyozalishwa katika msimu wa 2016/2017 kuwa ni Alizeti tani 182, Ufuta tani 32.5, karanga tani 50.7, Soya tani 134.56 na Mbaazi tani 46.4
Kuhusu pembejeo za kilimo,Nguaro anasema katika Msimu wa 2016/2017 wakulima walitumia pembejeo kiasi cha tani 19,450 za mbolea, kati ya hizo mbolea tani 173.8 zilikuwa ni za ruzuku ya Serikali na kwamba Pembejeo hizo zilitumika Katika mazao ya mahindi, kahawa na mpunga. Halmashauri ina maduka ya pembejeo za kilimo 45 na makampuni 5 ya pembejeo.
“Hali ya zana za kilimo za kisasa katika Halmashauri imeendelea kuboreshwa kwa wakulima mmoja mmoja na kwenye vikundi kwa kununua na kukopa matrekta 143 madogo na makubwa ambayo yanatumika kuongeza tija katika kilimo’’,anasema Nguaro.
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji,Afisa kilimo huyo analitaja eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kuwa ni lenye ukubwa wa hekta 2,000 na kwamba kati ya hizo jumla ya hekta 195 ndio zinalimwa sawa na asilimia 9.75.
Amesema hadi kufikia sasa kuna skimu tatu za umwagiliaji ambazo miundo mbinu yake imejengwa na zinafanya uzalishaji wa tani 375 za mpunga na tani 113 za viazi vitamu.
Rozina Chuwa ni Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Manispaa ya Songea ambapo anasema Halmashauri ya Manispaa ya Songea ina jumla ya Ng’ombe 5,341 kati ya hao ng’ombe 1,650 ni wa asili na ng’ombe 3,691 ni wa maziwa, aidha kuna nguruwe 3,692, Mbuzi 4,830, kondoo 98, kuku 810,157, mbwa 5,014, paka 286, kanga 820 na bata 1,102 hali hii itasaidia wananchi kupata lishe bora na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja.
Amesema Serikali imekuwa ikiboresha sekta ya mifugo kwa kujenga machinjio moja ya kisasa ambayo ipo katika hatua za mwisho za ujenzi na machinjio ndogondogo tatu ambazo zinafanya kazi na kwamba kuna Majosho saba ya kuogeshea Mbwa, kati ya hayo majosho matatu yanafanya kazi na Majosho manne hayafanyi kazi, pia yapo majosho manne ya kuogeshea ng’ombe ambayo yote hayafanyi kazi.
“Hadi mwishoni mwa mwezi Juni 2018 jumla ya ng’ombe 4,327 kati ya ng’ombe 5,673 walikuwa wamepigwa chapa ambao ni sawa na asilimia 90.15”,anasisitiza Chuwa.
Kuhusu sekta ya uvuvi,Chuwa anasema Halmshauri ya Manispaa ina jumla ya Mabwawa 552 ambayo hufugia samaki, vifaranga vya samaki hupatikana katika Mabwawa ya serikali yaliyopo eneo la Luhila kata ya Msamala na Mfugaji wa samaki hutumia gharama zao kununua vifaranga hao na kuwakuza katika mabwawa hivyo kuongea kipato kwa wananchi.
Imetolewa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Novemba 7,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa