UTAFITI uliofanywa mwaka 1999 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma unaonesha kuwa Manispaa hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji yanayotoka ardhini hali ambayo inasababisha kila mwaka visima kuendelea kukauka na kusababisha kero kwa wananchi.
Mhandisi wa Maji toka Mamlaka ya Maji safi Songea (SOUWASA) Mhandisi John Kapinga akizungumza na wananchi wa Kata ya Ruhuwiko wakati wa makabidhiano ya mradi wa maji wa Mtaa wa Ruhuwiko kanisani, amesema kuwa licha ya kuwepo kwa miradi ya uchimbaji visima,uchunguzi umebaini idadi ya visima imekuwa inaendelea kukauka kila mwaka na kusababisha uhaba wa maji kwa wananchi.
"Katika Manispaa ya Songea baaadhi ya maeneo vilichimbwa visima vyenye urefu wa meta 300 lakini hivi sasa vimekauka na havitoi maji kabisa'',anasisitiza Mhandisi Kapinga na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyopo ili kukabiliana na hatari ya kutoweka kwa maji ardhini na vyanzo vingine.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani WHO zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni mbili kutoka nchi zaidi ya 40 zenye mabonde ya mito wapo katika vita ya kugombania maji kutokana na uchafuzi wa vyanzo vya maji unaoendelea kwa kasi duniani kote.
WHO inalitaja tatizo la maji duniani kuongezeka zaidi miaka 50 ijayo na kusababisha vita kuu ya tatu ya Dunia ambayo itakuwa pia ya kugombania maji kwa kuwa idadi ya watu duniani inatarajia kuongezeka kutoka watu bilioni saba hivi sasa hadi kufikia bilioni 10.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Manispaa ya Songea
Mei 9,2018
SONGEA MUNICIPAL COUNCIL
Anuani ya Posta: P O BOX 14, SONGEA
Simu ya Mezani: 025 2602970
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@songeamc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Haki zote zimehifadhiwa